In Summary

Lakini uamuzi huo umefunikwa na wimbi la ukamataji wapigania haki za wanawake

Wanawake Saudi Arabia wajifunza kuendesha pikipiki baada ya marufuku kuondolewa

Nchi hiyo tajiri ya Kiarabu ilikuwa imepiga marufuku wanawake kuendesha magari na pikipiki, lakini mwaka jana iliondoa marufuku hiyo na sasa wanawake wameanza kujifunza kuendesha.

Hata mwaka mmoja uliopita, ilikuwa ni vigumu kuamini  mwanamke wa Saudi Arabia kuvaa suruali ya jeans inayobana pamoja na fulana ya Harley-Davidson-- akiendesha pikipiki mjini Riyadh kwenye viwanja vya michezo.

Lakini baada ya Juni 24 mwaka jana kuondoa marufuku hiyo ya kihistoria iliyodumu kwa miongo kadhaa ya kuzuia wanawake kuendesha, hivi sasa wanakusanyika kila wiki kwenye chuo binafsi cha kufundishia uendeshaji pikipiki cha Bikers Skills, kujifunza kuendesha.

Noura, ambaye alikataa kutaja jina lake halisi na ambaye ana umri wa miaka 31, alisema amekuwa akitamani kuendesha pikipiki kwa muda mrefu.

Kuondoa marufuku hiyo ambayo ilikuwa katika nchi ya Saudi Arabia peke yake na ambayo ilionyesha ukandamizwaji wa wanawake, ni moja ya mageuzi makubwa yanayofanywa na mtoto wa mfalme, Mohammed bin Salman.

Lakini uamuzi huo umefunikwa na wimbi la ukamataji wapigania haki za wanawake-- akiwemo mpambanaji mkongwe ambaye kwa muda mrefu amekuwa akipinga marufuku hiyo.

Hakuna msichana aliyekubali kuongea kuhusu marufuku hiyo katika kambi ya mazoezi ya usiku kutokana na suala hilo kuwa nyeti, badala yake walijikita katika haki za msingi ambazo wamenyimwa kwa muda mrefu.

Noura anasema alikuwa anakua akiona ndugu zake wakiendesha pikipiki.

Pembeni yake alikuwa msichana wa miaka 19, Leen Tinawi aliyekuwa akiendesha pikipiki aina ya Suzuki.

Kwa wanawake wote, kuendesha pikipiki ni kitu wanachokipenda na pia ni kama njia ya kuwsawezesha.

Wanafunzi hao wote wanamfuata mkufunzi kutoka Ukraine, Elena Bukaryeva, mwenye umri wa miaka 39 ambaye anaongoza Harley-Davidson.

Kwa siku nyingi, kituo hicho ni kwa ajili ya mashindano ya pikipiki ambayo hujumuisha wanaume tu.

Lakini tangu kianze kutoa mafunzo mwezi Februari, wanawake wanne wamejiunga na watatu kati yao ni raia wa Saudi Arabia, anasema Bukaryeva.

Maneno yake yanalingana na yaliyo katika matangazo ya kituo hicho yasemayo : "Ni zamu yako kuendesha."

Alipoulizwa sababu za wanawake kutojitokeza kwa wingi kujiunga na mafunzo hayo, ambayo yanagharimu dola 400 za Kimarekani, Bukaryeva alisema "labda ni kwa sababu familia zao zimewazuia."

Tinawi ana maoni kama hayo, akisema alikumbana na upinzani mkali kutoka familia yake.

Anasema wazazi wake walikuwa wakimwambia "unaendesha pikipiki, wewe ni msichana, ni hatari".

Nchi Saudi Arabia kuendesha pikipiki imekuwa ni kazi ya wanaume.

Hofu kubwa kwa wanawake katika kuendesha pikipiki imekuwa ni sheria ya mavazi.

Ndani ya chuo hicho, wanawake huvalia suruali za jeans zinazobana na kufunga kiunoni mtandio unaofika hadi magotini, lakini hiyo haiwezekani hadharani.