Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitarajia kuanza kutekeleza bajeti mpya, kumbukumbu zinaonyesha baadhi ya wizara hazikupata hata senti moja ya fedha za miradi ya maendeleo mwaka huu wa fedha.

Utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2017/18 unakamilika Juni 30 na ukusanyaji wa mapato na matumizi kwa mwaka mpya wa fedha utaanza kutekelezwa Julai Mosi.

Wakati maandalizi hayo yakiendelea kufanyiwa kazi, imebainika kuwa Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi pamoja na idara ya mawasiliano iliyo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano hazikupokea fedha zozote kutoka Hazina licha ya kuidhinishwa na bunge mwaka jana. Wakati wizara hizo zikikosa fedha za kufanikisha mipango ya maendeleo, nyingine nyingi zilipewa chini ya nusu ya kiasi kilichoidhinishwa.

Alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema kati ya Sh31.7 trilioni zilizoidhinishwa, Sh19.7 trilioni zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh11.9 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Kutotolewa kabisa kwa fedha za maendeleo kwa baadhi ya wizara huku nyingine zikipata chini ya matarajio ni suala ambalo limepigiwa kelele na wabunge, wachambuzi wa uchumi na wadau wa maendeleo kwamba linakwaza ufanikishaji wa mipango iliyowekwa.

Wabunge wengi walichangia mijadala ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara tofauti wakiitaka Serikali kuhakikisha inatekeleza yote yanayoridhiwa na Bunge kwa manufaa ya wananchi.

Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe alisema kutotolewa kwa fedha hizo kwa wakati kulichangiwa na Serikali kuelekeza fedha kwenye miradi ambayo haikuidhinishwa.

Mwaka huu wizara hiyo inayogusa maisha ya wananchi wengi iliidhinishiwa Sh35.6 bilioni na Sh4 bilioni zilikuwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Kwenye mawasiliano, mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya miundombinu, Moshi Kakoso alisema kutotolewa kwa fedha kulisimamisha utekelezaji wa miradi mingi.

“Kamati imegundua mpaka Machi mwaka huu, sekta ya mawasiliano haikupokea kiasi chochote kati ya Sh14 bilioni zilizotengwa na kuidhinishwa na Bunge,” alisema Kakoso.

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ni miongoni mwa zilizotengewa fedha nyingi mwaka huu. Zaidi ya Sh4.5 trilioni ziliidhinishwa kwa ajili ya matumizi yake ya kawaida na maendeleo.

Licha ya kuajiri zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania, sekta ya kilimo haikupewa kipaumbele kinachostahili kwenye utekelezaji wa bajeti. Kati ya Sh150 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, Wizara ya Kilimo ilipokea chini ya asilimia 20.

Taarifa za wizara hiyo zinaonyesha ilipokea Sh27.2 bilioni. Hata Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji mambo hayakuwa mazuri sana kwani ilipokea chini ya asilimia 40 ya fedha za maendeleo ilizotengewa. Kati ya Sh122 bilioni zilizopaswa kufanikisha miradi ya wizara hiyo, Hazina ilitoa Sh47 bilioni.

Wizara ya Mambo ya Ndani ilipokea Sh21.8 bilioni kati ya Sh40 bilioni wakati ile ya Nishati ikipata Sh424 bilioni kati ya Sh916 bilioni zilizoidhinishwa. Wizara ya Maji na Umwagiliaji ilipokea nusu ya bajeti iliyotengwa kwa ajili ya miradi yake. “Tunayo mipango mizuri sana lakini kunakuwa na ugumu kuitekeleza kutokana na ukosefu wa fedha,” alisema Mbunge wa Mlimba (Chadema), Suzan Kiwanga alipokuwa akichangia bajeti ya wizara hiyo mwezi uliopita.

Kwa mwaka 2017/18 wizara hiyo ilitengewa Sh623 bilioni, lakini mpaka Machi ilikuwa imepewa Sh347 bilioni.

Kutokana na hali hiyo, wabunge wengi waliochangia hoja ya wizara hiyo walisema suala hilo linadhihirisha kutokuwapo kwa nia ya dhati ya Serikali kumaliza uhaba wa maji unaowatesa wananchi katika maeneo mengi nchini.

Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika alilitaka Bunge kutopitisha bajeti hiyo na kupendekeza wizara ijipange upya ili kuleta mkakati wa kumaliza kero zinazowakabili wananchi muda mrefu.

“Suala hili linajadiliwa kwa miaka mingi. Tangu nimeingia kwenye Bunge hili wimbo umekuwa maji...maji...maji. Hii si haki kwa wapigakura wetu,” alisema Mnyika.

Licha ya Serikali kuipigia chapuo sera ya uchumi wa viwanda unaokusudia kuongeza ajira na kupunguza umaskini, Wakala wa wa Nishati Vijijini (Rea) haipewa fedha za kutosha kufikisha nishati hiyo maeneo yaliyokusudiwa.

Kutokana na umuhimu wa nishati kwenye uendeshaji wa viwanda na uzalishaji wa huduma tofauti za kijamii na kiuchumi, Spika wa Bunge, Job Ndugai aliitahadharisha na kuitaka Serikali kuchukua hatua.

“Waziri wa Fedha hili ni suala muhimu sana. Hakuna kitu ambacho Wizara ya Nishati inaweza kufanya kama haipati fedha zinazotakiwa, tena zilizoidhinishwa na Bunge,” alisema Ndugai.

Mwaka huu wa fedha, idara ya nishati iliyokuwa chini ya Wizara ya Nishati na Madini kabla ya kugawanywa na kuwa wizara mbili ilitengewa Sh945 bilioni lakini mpaka Machi ilikuwa imepokea Sh424 bilioni.

“Wakati mwingine tutaanza kuibana Wizara ya Fedha kama miradi ya maendeleo haitekelezwi kutokana na ukosefu wa fedha,” alisema Ndugai kipindi Bunge limekaa kama kamati kuidhinisha bajeti ya Wizara ya Kilimo.

Wachambuzi wa uchumi

Mchumi na mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar, Profesa Haji Semboja anasema Serikali inapaswa kuhakikisha makadirio yanayopendekezwa ni halisi ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Huwa inatokea mara nyingi. Kila mwaka kunakuwa na nakisi kwenye bajeti. Kuepuka hili, ipo haja ya kuwa na mango wa matumizi wenye uhalisia kulingana na rasilimali zilizopo,” alisema.

Mkurugenzi wa sera na utafiti wa Taasisi ya Repoa, Dk Abel Kinyondo anasema Serikali itakiwa kujifunza kutoka mataifa yaliyofanikiwa kutekeleza bajeti zao kwa uhakika akitoa mfano wa Botswana ambayo mara nyingi hukusanya mapato makubwa kuliko iliyopanga kuyatumia ndani ya mwaka husika wa fedha.

“Bajeti inatakiwa iwe halisi. Swali muhimu tunalotakiwa kujiuliza ni wapi tutapata fedha za ziada kufanikisha matumizi ambayo yanaongezeka kila siku. Kinyume na hapo tutaendelea kurudia kosa lilelile kila mwaka,” anashauri Dk Kinyondo.

Kama zilivyo nchi nyingine za Afrika Mashariki, bajeti ya mwaka huu wa fedha ilielekezwa kufanikisha utekelezaji wa Tanzania ya viwanda ili kuongeza ajira kwa vijana na kuunguza umaskini wa wananchi na Taifa kwa ujumla.