In Summary

Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina bungeni mjini Dodoma

Dodoma. Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeliomba Bunge kuidhinishia Sh56.45 bilioni katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2018/19, huku ikieleza kuwa fedha za maendeleo za bajeti ya wizara hiyo mwaka 2017/18, hadi kufikia Aprili 2018, zilikuwa hazijapokewa.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa wizara hiyo, Luhaga Mpina leo Mei 17, 2018 bungeni mjini Dodoma, kubainisha kuwa katika bajeti ya 2017/18 inayomalizika Juni 30, 2018, wizara hiyo iliidhinishiwa Sh6bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Amesema kuwa kati ya fedha hizo, Sh 4bilioni za matumizi ya maendeleo zilikuwa ni fedha za ndani kwa fungu la 99  ambalo ni sekta ya mifugo.

“Mpango wa Bajeti za maendeleo kwa kuendeleza kwa fungu 99 (Mifugo) ulihusisha utekelezaji wa Programu ya kufikia Aprili mwaka huu 2018 hakuna fedha iliyokuwa imetolewa,”amesema.

Kwa upande wa uvuvi , Mpina amesema katika mwaka wa fedha 2017/18, sekta ya uvuvi ilitengewa Sh2 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo lakini hadi kufikia Aprili mwaka huu hakuna fedha zilizotolewa.