In Summary

Wabunge hao wamelalamika kuhusu wizi na hujuma wanazofanyiwa wakulima na viongozi wa vyama hivyo.


Dodoma. Wabunge wameitaka Serikali kuviondoa vyama vya ushirika na kuruhusu uuzwaji wa mahindi nje ya nchi.

Hayo wameyasema leo jioni Mei 16, 2018 wakati wakichangia bajeti ya wizara ya kilimo ya mwaka 2018/19 bungeni jijini Dodoma.

Mbunge wa Magu (CCM), Kiswaga Destery amesema, “kuna tatizo, wananchi wanalalamika, wabunge wanalalamika, wananchi wamebaini wanaowapeleka katika ushirika ni sisi wabunge na viongozi.”

“Suala la ushirika wabunge wamelalamika wasikilizeni. Viongozi wa ushirika na wahasibu wametumia rushwa kupita, wanakwenda kuwaibia wakulima na wanunuzi wa pamba, mikataba tuliyonayo ni ya kukopa,” ameongeza.

Amesema, “viongozi wamechaguliwa na watu saba au kumi, bora wangechaguliwa na wananchi, mtawapa shida ma DC (wakuu wa wilaya), wakuu wa mikoa, hakuna kazi watakayokuwa wanaifanya zaidi ya kulinda wezi.”

Kuhusu zuio la mahindi, Destery amesema, “wabunge wanalalamika mahindi hapa, bila kuweka utaratibu yataoza, ni vizuri serikali ikafungua na mahindi haya yakiuzwa ndio mchango wenyewe na ndio maendeleo.”

Mbunge wa Mlimba (Chadema), Susan Kiwanga amesema, “inasikitisha sana kuona kilimo kinaachwa kiholela holela, unaanzaje kumzuia mtu asiuze nje, ninyi vipi mlitugea ninyi mtaji.”

Amesema wanapolima na kupata fedha “ndipo tunakwenda kuchangia huduma za jamii, sasa tunawezaje kujenga kama hatuna fedha.”

Kiwanga amesema, “huu ushirika ni kama janga la taifa, Serikali imechukua hatua gani kwa wale viongozi walioharibu ushirika, kama hamjachukua hatua mtawafunga wengi na mtagombana na wengi sana.”

Amesema bajeti ya kilimo iongezeke, masoko yawe wazi, mkulima aweze kuuza kokote na kama mnataka kudhibiti wekeni mazao yenu lakini si kwa fedha zake.

Mbunge wa Urambo (CCM), Margaret  Sitta amehoji kama wizara ya kilimo ina kalenda ya misimu ya kilimo kwa kila mkoa kwani imezoeleka mbolea kuwafikia wakulima kipindi cha kupalilia.

“Katika mazao yenye matatizo ni tumbaku, tumbaku inaiingizia nchi hii zaidi ya asilimia 40 ya fedha za kigeni. Hii changamoto tumekuwa tunazungumza kila tunapopata nafasi, tatizo ni nini,” amehoji Sitta