In Summary

Ni kutokana na wasanii wengi kuhudhuria msiba huo huku waombolezaji wakitaka kupiga nao picha


Mbeya.Shughuli za mazishi ya Masogange, imelazimika kusimama kwa muda baada waombolezaji jijini Mbeya kutaka kupiga picha na wasanii waliofika kijijini Utengule kwa baba yake atakapozikwa.

Masogange aliyefariki Aprili 20, akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Mama Ngoma, aliagwa jana Jumapili na mamia ya  watu katika viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam na baadaye kusafirishwa kuelekea Mbeya.

Katika safari hiyo baadhi ya wasanii wamejumuika na wadau mbalimbali wa masuala ya burudani.

Ujio wao katika msiba huo umekuwa ni neema pia kwa wakazi wa Kijiji cha Utengule na vitongoji vyake, ambao wamekuwa na shauku ya kuwaona wasanii hao macho kwa macho kwani wamekuwa wakiwaona kwenye televisheni na kuwasoma kwenye magazeti na mitandaoni.

MCL Digital ilishuhudia baadhi ya watu waliowekwa kwa ajili ya kulinda usalama eneo hilo wakiwatuliza watu waliokuwa wakisukumana kutaka kupiga picha na wasanii hadi ratiba kushindwa kuanza kwa wakati kama ilivyopangwa.

Shughuli za kuuaga mwili wa Masogange kijijini hapo zilitarajiwa kuanza saa 6:30 mpaka saa 7:00 na kuzikwa saa 7:30.