Juzi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo alieleza kwa uchungu jinsi viongozi wa kuteuliwa wanavyolalamikiwa kwa kukiuka sheria wakati wanapoadhibu madaktari badala ya kufuata taratibu.

Waziri Jafo alisema hayo katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa Afya uliofanyika jijini Dodoma, akiahidi kuwa ofisi yake itawaandikia viongozi wote wa kisiasa wa ngazi ya mkoa na wilaya kuwataka kufuata taratibu zilizopo badala ya kudhalilisha wataalamu hao hadharani.

Kauli hii si ya kwanza kwa kiongozi wa kitaifa kuizungumzia dhidi ya vitendo hivyo vinavyozidi kukua kila kona na kila kukicha. Juzi, Waziri Jafo alizungumzia udhalilishaji wa madaktari, lakini ukweli ni kwamba watu wa kila fani na kila kada wanadhalilishwa kwa kupewa adhabu hizo hadharani na bila ya kufuata taratibu zilizopo.

Imefikia wakati sasa inaonekana kwamba viongozi wa kuteuliwa, hasa wa wakuu wa mikoa na wa wilaya wanayo mamlaka ya kufanya lolote bila ya kujali sheria na taratibu zilizopo.

Imefikia hatua hata ile sheria iliyoundwa kwa ajili ya kudhibiti mtu ambaye anaweza kuvuruga amani kwa kumuweka ndani kwa kipindi kisichozidi saa 48, sasa inatumika kama adhabu kwamba mtu akikosea anawekwa ndani kwa muda huo.

Kwa hiyo mamlaka zilizowekwa kwa ajili ya kushughulikia watumishi wa umma, hazina kazi tena na vyombo vya dola vilivyowekwa kwa ajili ya kusimamia haki, sasa vinaamrishwa viadhibu badala ya kupeleka watuhumiwa mbele ya mkono wa sheria.

Hili ni suala ambalo linazungumzwa kila kukicha, lakini inaonekana baadhi ya wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa wamelipuuza na wanaendelea na kujichukulia hatua ambazo kwa kiasi fulani hazisaidii kurekebisha jamii kwa kuwa zinapokewa kwa hisia hasi.

Juzi, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga aliagiza kukamatwa kwa maofisa watendaji wa vijiji vya Endesh, Mongay na Tumati kwa kosa la kuzuia maji yasiende katika Kijiji cha Dongobesh na kusababisha uhaba wa maji.

Mofuga alitoa agizo hilo jana akiwa katika ziara ya kukagua miundombinu ya maji na ujenzi wa kituo cha afya cha Dongobesh na kupokea malalamiko kutoka kwa wakazi wa eneo hilo waliolalamikia tabia ya baadhi ya wanavijiji hivyo kuharibu miundombinu ya maji na kumwagilia mashamba yao huku wao wakikosa huduma hiyo muhimu.

Baada ya kusikiliza malalamiko hayo alionana na viongozi wa vijiji hivyo, lakini hakufanikiwa kuwapata na kuagiza wakamatwe.

Tukio hilo ni moja kati ya mengi yanayotokea sehemu mbalimbali, baadhi yanaripotiwa na baadhi hayaripotiwi lakini kilicho dhahiri ni kwamba wananchi wanaumia na hawawezi kuchukua hatua dhidi ya viongozi wa kuteuliwa kwa kuwa hawana mamlaka juu yao.

Serikali haina budi kukomesha mwenendo huu kwa kuwa nchi ilishajiwekea utaratibu wake wa kuadhibu wakosaji makazini na wanaovunja sheria za nchi. Kuachia utaratibu huu uendelee ni kuendelea kuwanyanyasa wanyonge ambao hawana mamlaka dhidi ya viongozi wa kuteuliwa ambao wana sauti kwenye vyombo vya dola.

Kiongozi bora ni yule anayeangalia utaratibu wa utendaji kazi, ukoje na kufikiria njia za kuuboresha badala ya kukimbilia kuadhibu kwa kutumia sheria zinazotungwa kwa madhumuni mengine.

Kiongozi bora pia anatakiwa kutumia mamlaka na taratibu zilizowekwa kisheria na zilizoundwa kwa kutumia kodi za wananchi, kuadhibu wale wanaoonekana kuvunja sheria.

Kutotumia vitu hivyo kunatoa mwanya kwa viongozi wa kuteuliwa kuadhibu hata watu ambao wana tofauti ambazo si za masilahi mapana ya kitaifa. Uvunjwaji huu wa sheria na taratibu ukomeshwe.