In Summary
  • Uwekezaji kwenye mradi wa gesi asilia unahitaji fedha nyingi itakayofanikisha ununuzi wa mitambo inayotumia teknolojia ya kisasa. Fedha hizo ni muhimu pia kwa ajili ya kuwalipa wataalamu pamoja na mambo mengine. Kufanikisha uwekezaji huo, kampuni nyingi zaidi, ndani na nje ya nchi, zikaribishwe kuwekeza.

Kubuni na kujenga mradi mgumu wenye vipengele vingi wa gesi asilia iliyosindikwa Tanzania (TGP) kunahitaji mipango makini, mkakati uliothibitishwa na matumizi ya teknolojia mbalimbali za kisasa.

Mradi huu utakuwa mkubwa zaidi kati ya miundombinu iliyowahi kujengwa katika historia ya Tanzania mpaka sasa ukiwa na uwezo wa kuleta mabadiliko ya uchumi nchini.

Hata hivyo, hayo yote yatatimia kama kutakuwa na miundombinu sahihi kutokana na mchakato wa masuala mbalimbali unaoendelea.

Hivyo basi, ni muhimu kuzingatia teknolojia itakayotumika kuufanikisha mradi huo na kujiandaa kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza katika kila hatua ya utekelezaji wake kuhakikisha unakuwa na mafanikio yaliyokusudiwa.

Katika ujenzi wake, baadhi ya kampuni zenye majina mkubwa na uzoefu wa muda mrefu katika biashara ya mafuta, petroli na gesi kama Shell, ExxonMobil na Statoil zinahusika.

Kila moja ina hazina ya utaalamu itakaoutumia kufanikisha majukumu yake kati ya mengi yanayoendelea kutekelezwa.

Hizi ni kampuni ambazo zimekamilisha miradi ya LNG kwa mafanikio katika maeneo mengi duniani, lakini bado zinavutiwa na hazina ya gesi iliyogundulika Tanzania.

Kujaribu kuchimba nishati yoyote ni mchakato unaohitaji taratibu zilizopimwa na zana stahiki.

Kupata gesi asilia kwa njia salama ni jambo gumu na tete wakati wote lakini kwa mradi wa TGP kuna vikwazo vingine vingi unavyotakiwa kuvitatua.

Akiba kubwa ya gesi ya Tanzania ya zaidi ya futi 57.25 trilioni za ujazo, ipo kina kirefu chini ya Bahari ya Hindi. Kati ya hazina hiyo, takriban futi trilioni 49.5 za ujazo zipo baharini.

Siyo kwamba hazina yote hiyo ipo chini sana ya sakafu ya bahari, sehemu yake inapatikana mita 2,500 ya kina cha maji lakini baadhi ya maeneo ni umbali wa kilomita 100 kutoka ufukweni.

Kama hiyo haitoshi, sakafu ya bahari ina mifumo mingi ya makorongo, hivyo kufanya uchimbaji wa gesi kuwa mgumu zaidi.

Japokuwa kampuni kama Shell zimejenga miradi mbalimbali ya LNG maeneo mengi mengine duniani, Tanzania inatoa changamoto mpya na ya tofauti kabisa. Vifaa maalumu vya uchimbaji na uzalishaji vitahitajika kuhuishwa ili kufanya kazi katika mazingira ya asili ya kipekee.

Uchimbaji wa gesi unahitaji matumizi ya juu ya teknolojia. Hata baada ya hapo, kusindika na kuihifadhi gesi baada ya kuchimbwa hatimaye kusafirishwa nje ya nchi kunahitaji mchango mkubwa wa kiufundi.

Mpango uliopo sasa ni kujenga kituo cha kuhifadhi LNG nchi kavu katika Kijiji cha Likong’o mjini Lindi katika ufukwe wa Bahari ya Hindi. Utakapokamilika utaiwezesha Tanzania kusafirisha gesi asilia duniani kote.

Uwekezaji huu katika miundobinu utakuwa na uwezo wa kujenga na kupanua viwanda vingine mbalimbali nchini, hivyo kukuza zaidi uchumi wa Taifa na kupunguza umaskini kwa wananchi.

Ni kweli kwamba mambo haya hayawezi kutokea bila ya uwekezaji wa kutosha. Teknolojia ya juu ina gharama kubwa. Licha ya kuthibitika kuwa mradi ni wa faida na kutangaza uwezo wake kwa miaka mingi ijayo, litakuwa jambo muhimu kuondoa mashaka yoyote ama kwa Serikali au mwekezaji.

LNG ni maendeleo na ubunifu muhimu kwa mustakabali wa uzalishaji wa nishati duniani unaoambatana na fursa kubwa zinazopatikana kwa kampuni na Serikali ambazo zinatengeneza miundombinu sahihi na kufanikisha usafirishaji kwa ufanisi, kabla rasilimali hii ya thamani haijafika kwenye soko lililokusudiwa.

Kampuni kubwa za mafuta zinaamini LNG ni sekta muhimu kuwekeza. Kampuni ya Shell, kwa mfano, hivi karibuni imemaliza kubuni na kujenga meli ya Prelude, kiwanda cha LNG kinachoelea ambacho wakati naandika makala haya ndicho kikubwa zaidi baharini.

Wachambuzi wakakadiria gharama za kujenga meli hiyo ni takriban Dola 12.6 bilioni za Marekani. Hiki si kiasi cha fedha ambacho kampuni yoyote inaweza kutumia isipokuwa pale ambapo wana uhakika wa kupata faida kubwa siku zijazo.

Takwimu za Shirika la Kimataifa la Nishati zinaonyesha mahitaji ya gesi asilia duniani yanaweza kuongezeka kwa zaidi ya nusu ifikapo mwaka 2040 na mradi wa TGP utaifanya Tanzania kuwa kitovu cha usambazaji wa LNG.

Iwapo Tanzania itaweza kufanya uwekezaji wa kutosha kwa ushirikiano wa Serikali na wawekezaji wakubwa kama vile Shell, Statoil, ExxonMobil, Ophir Energy na Pavilion Energy huku ikihakikisha kila mhusika anaelewa, kutambua na kukubaliana na vigezo, basi mradi utakuwa katika njia sahihi ya kufanya mageuzi ya bidhaa zinazosafirishwa nje jambo litakalosaidia kuboresha maisha ya wananchi.