In Summary
  • Wakizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo inayoendeshwa na halmashauri ya wilaya ya Misungwi kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la kivulini jijini hapa, kila upande uliainisha udhaifu wa mwingine.

Misungwi. Wanawake na wanaume wilayani Misungwi jana wametumia kampeni ya kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji kijinsia kwa kulaumiana huku kila upande ukiushutumu mwingine kusababisha vitendo hivyo.

Wakizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo inayoendeshwa na halmashauri ya wilaya ya Misungwi kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la kivulini jijini hapa, kila upande uliainisha udhaifu wa mwingine.

Fransisco Kiyumbi alidai kuwa baadhi ya wanawake huwafanyia waume zao ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa kuwanyima chakula na unyumba pindi wanaposikia waume zao wana uhusiano nje ya ndoa.

Kiyumbi alisema baadhi ya wanawake huuza mazao na kununua vito vya thamani, vipodozi na nguo za gharama bila kujali akiba ya chakula kwa familia.

“Wanaficha mazao kwenye ndoo wakijifanya wanaenda kuteka maji na kwenda kuuza ili wanunue vipodozi, vito vya thamani na nguo za gharama; wanaishi maisha ya kushindana na wenzao bila kujali uwezo wao kiuchumi,” alisema Kitumbi.

Regina Kubunga alijibu madai hayo kwa kutaja udhaifu wa wanaume ikiwamo baadhi yao kutotimiza wajibu wao kwenye familia.

Alisema kwamba wanawake hulazimika kutumia akili na mbinu mbadala kutafuta fedha za kugharamia chakula na mahitaji mengine ya familia ikiwamo elimu ya watoto, huku wanaume kwa upande wao wakiwa hawatoi chochote.