In Summary
  • Tozo zinazopendekezwa kufutwa ni pamoja na ada katika zao la chai, kahawa, tumbaku, sukari na pamba. Kwa mujibu wa wizara hiyo, lengo la kufuta kwa tozo hizo ni kuimarisha upatikanaji wa pembejeo. Pia, imependekeza kufutwa kwa tozo tano kwenye uzalishaji wa mbegu na kwa ajili ya kuimarisha maendeleo ya ushirika nchini huku sita zikiwa katika ngazi za ushirika.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2018/19, waziri mwenye dhamana, Dk Charles Tizeba amependekeza kufutwa kwa ada na tozo 21 katika mazao, uzalishaji wa mbegu na vyama vya ushirika ambazo zimeonekana kuwa kero kwa maendeleo ya sekta ya kilimo.

Tozo zinazopendekezwa kufutwa ni pamoja na ada katika zao la chai, kahawa, tumbaku, sukari na pamba. Kwa mujibu wa wizara hiyo, lengo la kufuta kwa tozo hizo ni kuimarisha upatikanaji wa pembejeo. Pia, imependekeza kufutwa kwa tozo tano kwenye uzalishaji wa mbegu na kwa ajili ya kuimarisha maendeleo ya ushirika nchini huku sita zikiwa katika ngazi za ushirika.

Wizara hiyo pia imeahidi kuendelea kuchambua na kubaini ada na tozo ambazo bado ni kero kwa wakulima nchini na kuzifuta, lengo likiwa kubakiza zile ambazo zina uhusiano wa moja kwa moja na uendelezaji wa mazao husika kama uendelezaji wa utafiti wa mazao.

Huo ni mwendelezo wa wizara hiyo kutoa unafuu kwa wakulima kwani katika bajeti iliyopita ilifuta kodi, ada na tozo 80 kati ya 139 za mazao ya kilimo huku ikipunguza viwango vinne vya tozo ambavyo vilionekana kuwa kero.

Tunaipongeza Serikali kwa hatua hiyo muhimu katika sekta ya kilimo tukiamini kwamba itatoa unafuu wa kodi katika vifungashio vya mazao na mbegu za mazao ya kilimo, mabomba ya kunyunyuzia dawa, mashine na mitambo ya usindikaji wa mazao, miundombinu ya uzalishaji na hifadhi ya mazao ya bustani na kulinda wazalishaji wa ndani dhidi ya ushindani usio sawa na bidhaa kutoka nje ya nchi.

Tunaamini unafuu huo hautaishia hapo, badala yake itaendelea kuhakikisha kero zote zinazokwamisha maendeleo ya mazao ya kilimo zinashughulikiwa.

Tunaamini pamoja na kufuta tozo hizo, bado kuna changamoto kadhaa katika sekta hiyo ikiwamo ubadhirifu wa mali katika vyama vya ushirika unaofanywa na watendaji wa vyama wasio waaminifu lakini pia uelewa mdogo juu ya haki, wajibu na majukumu yao kama wamiliki wa vyama.

Hivyo, tunaiomba Serikali kuimarisha usimamizi kwa kuongeza kasi ya ukaguzi wa vyama lakini pia kuwajengea uwezo viongozi na kutoa mafunzo kwa wanachama kuhusu haki na wajibu wao.

Sambamba hayo, tunaitaka Serikali ishirikiane na wadau wengine kuwasaidia wakulima ili wapate masoko ya uhakika na bei nzuri ili kuwajengea na hamasa ya kuongeza tija katika kazi hiyo ambayo ni uti wa mgongo wa Taifa.

Zipo jitihada za kuboresha miundombinu hasa ya kusafirisha mazao yao kwa urahisi, tunashauri hilo lifanywe kwa nguvu zaidi kwani ni moja ya vikwazo vya kufikia masoko hasa ya ndani na yale ya uhakika.

Changamoto nyingine inayowakabili wakulima ni kuongeza thamani ya mazao yao. Wapo wanaojipinda na kulima maeneo makubwa na kupata mavuno mengi lakini yanayoishia kuozea shambani kutokana na sababu nyingi ikiwamo masoko.

Wito wetu ni Serikali na wadau kuwa na mkakati mkubwa wa kubuni, kununua na kusambaza teknolojia rahisi za usindikaji wa mazao.

Hili likifanikiwa, itakuwa rahisi kwao kuuza bidhaa zilizoongezewa thamani na ambazo utunzaji wake utakuwa rahisi.