In Summary

Kauli za wabunge hao walizozitoa katika mjadala wa bajeti ya wizara hiyo ya Sh170.2 bilioni iliyojadiliwa kwa siku mbili zilionekana kumtikisa Dk Tizeba ambaye jana jioni wakati akijibu hoja za wabunge alisema hakutakuwa na kizuizi tena kwa wakulima kuuza mazao yao nje ya nchi.

Dodoma. Wabunge bila kujali itikadi zao, jana walimbana waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba na kuitaka Serikali kuiondoa bungeni bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2018/19 ili kuja na nyingine inayojibu maisha ya Watanzania.

Kauli za wabunge hao walizozitoa katika mjadala wa bajeti ya wizara hiyo ya Sh170.2 bilioni iliyojadiliwa kwa siku mbili zilionekana kumtikisa Dk Tizeba ambaye jana jioni wakati akijibu hoja za wabunge alisema hakutakuwa na kizuizi tena kwa wakulima kuuza mazao yao nje ya nchi.

Katika mjadala huo, wabunge saba wa CCM walitamka wazi kutoiunga mkono, baadhi wakimponda Dk Tizeba na kumuomba Rais John Magufuli kumchukulia hatua.

Wabunge waichambua bajeti

Walioipinga bajeti hiyo kwa maelezo ya kutokuwa na majibu ya kilio cha wakulima ni Ignas Malocha (Kwela), Richard Ndassa (Sumve), Jacqueline Ngonyani (viti maalumu), Joseph Msukuma (Geita Vijijini), Hussein Bashe (Nzega Mjini), Nape Nnauye (Mtama) na Mashimba Ndaki wa Maswa Magharibi.

Bajeti hiyo ambayo ni pungufu kwa asilimia 23 ikilinganishwa na ya mwaka 2017/18 ya Sh221 bilioni, ilipitishwa jana jioni.

Hoja za wabunge katika mjadala wa bajeti hiyo zilikuwa ni kutengwa kwa fedha kiduchu za maendeleo wakati asilimia 75 ya Watanzania ni wakulima, vyama vya ushirika kutuhumiwa kuwanyonya wakulima, ucheleweshwaji wa mbolea, zuio la Serikali kuuza mazao nje ya nchi, bei ya zao la pamba kushuka kutoka Sh1,200 hadi Sh1,100 na madai ya mawakala wa pembejeo za kilimo kutolipwa.

Bashe na Nape waliitaka Serikali kuiondoa bajeti hiyo bungeni na kwenda kujipanga upya, hoja ambayo ilikosolewa na mbunge wa Bariadi (CCM), Andrew Chenge aliyependekeza kanuni ya Bunge kutumika ili kuifanyia marekebisho katika maeneno yanayolalamikiwa.

Chenge alisema hoja ya Bashe ya kutumia kanuni ya 69 kuirudisha bajeti hiyo kwa wizara za Kilimo na Fedha kwenda kuiweka sawa ni nzuri, lakini akashauri kanuni ya 105 itumike ili kuifanyia marekebisho na sio kuiondoa.

Chenge ambaye pia ni mwenyekiti wa Bunge alisema Wizara ya Kilimo ina idadi kubwa ya wasomi, lakini katika bajeti hiyo anaona fedha za maendeleo zinakwenda chini.

Kuhusu sakata la pamba ambalo juzi Ndassa na Ndaki walipinga na ndio sababu ya kutoiunga mkono kwa upande wake, Chenge alisema, “mimi nimekulia katika zao hili (pamba), Afrika nzima walikuwa wanakuja wanajifunza Tanzania, tulivuruga wenyewe, mimi kama kiongozi wa Bariadi sitakubali utaratibu unaopendekezwa na Serikali.”

Utaratibu ambao Chenge na wabunge wengine wanaotoka mikoa inayolima zao hilo waliupinga ni wa kuuza zao hilo kwa mfumo wa ushirika na badala yake mkulima akauze mwenyewe sokoni huku wakitaka Sh100 iliyopunguzwa kwa kila kilo irudishwe.

Katika hoja yake Bashe, aliwaomba wabunge wote kuungana kuikataa bajeti hiyo ili wizara ikajipange na kuja na nyingine inayogusa maisha ya watu kwani haiwezekani fedha za maendeleo zikapungua kwa asilimia 34.

“Nataka niwaombe wabunge bajeti hii tutumie kanuni ya 69 tuirudishe Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha zikakae iweze kuja na bajeti inayogusa maisha ya watu,” alisema Bashe.

“Tumeandaa bajeti ya Sh32 trilioni, Sh12 trilioni ni fedha za maendeleo, sekta ya kilimo inachangia wastani wa asilimia 30 ya pato la Taifa, bajeti ya maendeleo ya sekta ya kilimo ni Sh94 bilioni, ambayo ni sawa sawa na asilimia 0.8 ya ‘total’ bajeti ya ‘development.”

“Bajeti ya maendeleo, kweli sekta inayochangia asilimia 30 ndiyo inayotengewa chini ya asilimia moja ya bajeti nzima ya maendeleo, sekta ambayo inaajiri wastani wa asilimia 60 hadi 65 ya ajira za Watanzani chini ya asimilia moja, inasambaza malighafi katika viwanda kwa asilimia 70.”

“Jambo la kusikitisha ni kuwa sekta hii imeendelea kuonewa katika nchi yetu na sio sahihi, wabunge hawa wa CCM tunawajibu wa kumlinda mkulima, naomba bajeti hii irudishwe ili (Wakala wa Taifa wa Chakula) NRF apewe fedha alizoomba na masharti ya kusafirisha mazao kwenda kuuza nje yaondolewe.”

Mbunge huyo aliungwa mkono na Nape aliyeitaka Serikali kutoona aibu kuiondoa bajeti hiyo ili wakajipange upya kwa kuwa inakwenda kuiumiza Serikali. Pia, mbunge huyo alihoji ziliko fedha nyingi ambazo Serikali imekuwa ikijigamba kuwa imekusanya kwa kiasi kikubwa wakati hakuna pesa katika miradi ya maendeleo.

“Sasa tunayo nafasi ya ujumbe tunaotaka kupeleka kwenye umma, ujumbe kwamba tunajali maendeleo ya vitu au maendeleo ya watu ambao ndio waliotuweka madarakani,” alisema Nape.

“Wakati fulani tulisema kuwa Serikali ikwepe kuwekeza fedha nyingi kwenye miradi mikubwa inayoweza kujiendesha kibiashara, lakini tukashambuliwa kama si wazalendo katika nchi hii na hili Tizeba tutakubebesha bure, lakini si lako.”

Nape alisema ilani ya uchaguzi ya CCM ilitamka kuwa Serikali itakayoundwa itakuwa na jukumu la kuwasaidia wakulima kutafuta masoko nje, lakini kwa sasa imekuwa kinyume na ilani hiyo, hivyo kukaa mezani ndiyo suluhu.

Akichangia kwa sauti ya juu huku wabunge wa CCM wakiwa kimya na wale wa upinzani wakishangilia, Nape alihoji, “ukimwambia mtu akale magunia 20 ya mbaazi si unamtukana huyu, hivi tunawaambia nini wakulima katika jambo hili, ni kwa nini tusiwe wepesi wa kukubali ushauri na kuzungumza kwa pamoja.”

Tizeba, Mwijage hawatoshi

Mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya na Rashid Shangazi wa Mlalo (CCM) walisema Dk Tizeba na waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage wameshindwa kazi na kumtaka Rais John Magufuli awaangalie.

Sakaya alisema, “kama tunataka kwenda katika uchumi wa viwanda, lazima Serikali ijidhatiti katika kilimo, ukiangalia dhamira hazioani. Hatuwezi kwenda kama hatuweki jitihada za kilimo.”

Kwa upande wake, Shangazi alianza kwa kusema Rais Magufuli aliwahi kusema kuna wateule wake ambao hawamwelewi

“Nafikiri mawaziri Tizeba na Mwijage hawamwelewi,” alisema.

“Kama tunakusudia kuwa na Tanzania ya viwanda halafu hatujui tunataka nini itakuwa ni kifo, wakati Tanzania inapata uhuru Mwalimu Julius Nyerere alianzisha mazao ya kimkakati na viwanda, lakini hili limeshindikana kwa sasa.”

Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Aeshi Hillay aligusia kile kilichochangiwa na wabunge wengi kuhusu madai ya mawakala akiitaka Serikali, hususan waziri wa Fedha alieleze Bunge kama wanastahili kulipwa au la, kwa kuwa yamekuwapo madai ya muda mrefu na baadhi wamekufa pasipo kupata stahiki zao huku wengine mali zao zikiwamo nyumba zikiuzwa na taasisi za fedha kufidia mikopo.

Majibu ya Dk Tizeba

Akizungumza wakati akijibu hoja za wabunge, Dk Tizeba alisema milango iko wazi na hakutakuwa na kizuizi kwa wakulima kuuza mazao yao nje ya nchi.

Alisema kwa sasa wakulima wanatakiwa kuwa makini kwa kutouza mazao yote ili chakula kiweze kutosheleza nchi.

Waziri huyo alisema Serikali imeweka mipango mizuri kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wa mazao ambayo yanapata masoko nje ya nchi, huku akiwatoa hofu wabunge kuwa Serikali itawasaidia.

Kuhusu pamba, Dk Tizeba alisema Serikali iko makini zaidi katika ununuzi wa zao hilo na hakuna mahali walipotangaza kuwa itanunuliwa kupitia vyama vya ushirika, hivyo akawataka wabunge kutokuwa na hofu.

“Hata hivyo hakuna sheria ya kuwazuia kununua pamba au zao lolote vyama vya ushirika, bali wanatakiwa kuwa na fedha zao wenyewe sio kutegemea fedha za wafanyabiashara. Naomba watuamini,” alisema Dk Tizeba

Kuhusu bajeti ya wizara hiyo kuwa ndogo, alisisitiza kwamba hakutakuwa na shida yoyote kwa maelezo kuwa wizara hiyo ni mtambuka na inasimamiwa na zaidi ya wizara tatu ikiwamo Tamisemi.

Nape amkomalia Tizeba

Hata hivyo, kabla ya bajeti ya wizara hii kupitishwa mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, alinusuru shilingi kung’ang’aniwa katika mshahara wa wazi Tizeba, kutokana na Nape kutoridhishwa na majibu ya Serikali kuhusu fedha zinazotokana na ushuru wa mauzo ya nje ya nchi kwa zao la korosho.

Awali, Nape aliomba maelezo ya Serikali kwenye pembejeo za korosho na pia mauzo ya nje ya nchi na alisema majibu yasimpomridhisha angekamata shilingi. Katika majibu yake, Dk Tizeba alisema Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhusu kupatikana kwa ‘sulphur’ katika mikorosho.

Hata hivyo jibu hilo na maelezo mengine ya Dk Tizeba hayakumridhisha Nape na kutoa hoja ili wabunge wenzake wachangie jambo hilo, ambapo wabunge kadhaa walichangia.

Licha ya waziri Jenister Mhagama (Ofisi ya Waziri Mkuu) na naibu waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji kusaidia majibu ya hoja hiyo, lakini mwisho alikuwa ni Mhagama aliyesaidia kwa kumtaka Nape kuwasilisha hoja hiyo katika Kamati ya Bunge ya Bajeti ili ikajadiliwe huko, suala ambalo Zungu aliliunga mkono na kumtaka Nape kuwasilisha hoja hiyo kesho, jambo ambalo pia Nape aliliafiki.

Nyongeza na Habel Chidawali