In Summary
  • Binafsi sifahamu kosa la kukamatwa kwa kijana huyo, tuhuma zinazomkabili au kama ameshtakiwa basi ni kwa kosa lipi. Hivyo si nia yangu kuzungumzia tuhuma zinazomkabili kijana huyo.

Kumekuwa na video inayozunguka katika mitandao ya kijamii inayomuonyesha kijana akihojiwa na ofisa wa polisi juu ya mchoro uliopo mwilini mwake (tattoo).

Binafsi sifahamu kosa la kukamatwa kwa kijana huyo, tuhuma zinazomkabili au kama ameshtakiwa basi ni kwa kosa lipi. Hivyo si nia yangu kuzungumzia tuhuma zinazomkabili kijana huyo.

Tukumbuke kuwa tattoo ni fani inayoingiza mamilioni ya dola za Marekani katika dunia hii na imekuwa ikitanuka kwa kasi hasa ukizingatia nyota wa filamu, michezo na sanaa nyingine huitangaza bure kwa michoro inayochorwa katika miili yao.

Hapa Tanzania hatujabaki nyuma kwani vijana wanajicharaza nembo kwa picha katika miili yao. Jambo Hili linagusa maeneo ya maadili, afya na utawala wa sanaa. Swali la kujiuliza ni je, vyombo vya usimamizi wa sheria kama polisi vinaijua vizuri kisheria sanaa ya tattoo.

Kwanza tufahamu tattoo ni nini? Hii ni sehemu ya fani ya sanaa za ufundi inayogeuza mwili wa binadamu kuwa malighafi au kitambaa (turubai/canvas) ya kuchorea.

Tattoo ni urembo na utambulisho hutumika kuonyesha cheo (social status) kama nembo ya kujivunia. Ni alama katika jamii (kama chanjo) na hata makabila kadhaa kama sehemu ya ibada au tiba za kiasili.

Uchoraji wa tattoo ni tamaduni za siku nyingi za Mwafrika na Mtanzania. Makabila mengi ya Tanzania kama Wamakomde, Wasukuma, Wamang’ati, Wasonjo, Wambulu, Wangindo, Wandengereko, Wabarbeig na wengine wengi wanatumia katika tamaduni zao.

Hata katika makabila yasiyo na tattoo za jumla kwa watu wake wanazo kwa makundi maalumu kama machifu, waganga, majemedari, wanikulu na kadhalika.

Tattoo za kisasa ziliongezewa umaarufu na mabaharia miaka ya 1980 na mwendelezo wake ndio huu wa leo.

Upo ubishani kwenye tasnia ya sanaa baadhi ya wadau wakidai uchongaji meno ni sehemu ya sanaa ya tattoo na wengine kuwa ni sehemu ya sanaa ya uchongaji ama pia baadhi hudai sanaa zote mbili zinahusika

Aina za tattoo

Zipo aina mbili za tattoo; za kudumu na za muda. Kupaka hina ni ya muda. Kutoga pua, masikio na sehemu nyingine za mwili, kuchanja chale, ndonya kama za Wagogo na Wamakonde, kutengeneza makovu (scarification) ni baadhi ya tattoo za kudumu.

Pia zipo tattoo za kimatibabu kama chanjo za ndui, operesheni na uwekaji alama mwilini kwa ajili ya matibabu ya baadaye.

Ni kazi ya wananchi, Serikali na wadau wengine kuheshimu na kuendeleza mila za Kitanzania. Na hata katika kujenga uzalendo ambao ni kampeni ya Serikali ya Awamu ya Tano iliyozinduliwa rasmi na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Desemba 8, 2017.

Utamaduni ni sehemu muhimu ya kampeni hiyo. Lakini katika kuendeleza sanaa hii tunahitaji kuweka mazingira mapya yanayoendana na hali ya sasa.

Katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa na muingiliano wa tamaduni, ni muhimu kwa Serikali na taasisi zake kushirikiana na wadau wa kisekta katika kupata maelewano juu ya njia bora za kuendeleza Taifa.

Moja ya kazi za Serikali ni kutunga sheria au kufanya marekebisho ya sheria yanayoweza kuweka mipaka, kuongoza na kutoa adhabu kwenye sanaa hii ili uandikaji wa tattoo uwe salama zaidi na kuepukana na athari zinazoweza kutokea.

Tattoo na maadili

Lipo tatizo la msingi la kugeuza maadili kuwa ‘madili’. Maana yake ni tabia ya kurukia kulaumu na kutoa adhabu linapotokea tatizo badala ya kurudi nyuma na kuangalia malezi ya vijana wetu majumbani na katika mifumo rasmi au shuleni.

Lakini kwa sababu maadili hubadilika, basi kuna haja ya kuwa na mfumo wa kufanya tathmini wa maadili na kuyaweka wazi kwa kuyaandika pale inapowezekana.

Tattoo kama zilivyo nyanja zingine za kisanii zinakaguliwa na maadili ya jamii husika. Kwa mfano, kuandika matusi dhidi ya mtu mwingine kwenye tattoo ni makosa na ikithibitika mahakamani hatua za kisheria zinaweza kuchukuliwa.

Vilevile kuandika tattoo kwa kulazimisha linaweza kuwa kosa la jinai. Iwe marufuku kumlazimisha mtu mwingine kuwa na tattoo kwani ni kumnyang’anya haki yake ya msingi.

Tukumbuke kuwa mila za baadhi ya makabila huko nyuma zilishinikiza na hata kulazimisha uwekwaji wa tattoo kwa wanajamii wao. Kwa mazingira ya sasa mila hizo zina haja ya kuangaliwa upya.

Ipo haja ya msingi ya kulinda watoto dhidi ya uchoraji tattoo hasa zile za kudumu. Ili mtoto achorwe tattoo sharti mzazi au mlezi kuwapo wakati wa uchoraji wa tattoo za muda kama hina kwa watoto.