In Summary
  • Yako mengi ya kukumbukwa kuhusu utendaji wa kizalendo aliokuwa nao Sokoine aliyefariki dunia mwaka 1984 akiwa na umri mdogo wa miaka 45, lakini kubwa ni namna alivyotilia mkazo kilimo. Sokoine aliamini kuwa ‘siasa ni kilimo’ na ndiyo maana siku zote aliipigania sekta hiyo kwa kauli na vitendo.

Juzi, Aprili 12 ilikuwa kumbukumbu ya miaka 34 tangu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Sokoine alipofariki dunia kwa ajali ya gari wakati akitokea mjini Dodoma baada ya kumalizika kikao cha Bunge alichokuwa akihudhuria.

Yako mengi ya kukumbukwa kuhusu utendaji wa kizalendo aliokuwa nao Sokoine aliyefariki dunia mwaka 1984 akiwa na umri mdogo wa miaka 45, lakini kubwa ni namna alivyotilia mkazo kilimo. Sokoine aliamini kuwa ‘siasa ni kilimo’ na ndiyo maana siku zote aliipigania sekta hiyo kwa kauli na vitendo.

Kiongozi huyo mchapakazi, ndoto yake ilikuwa ni kutaka Tanzania ijitosheleze yenyewe kwa chakula, na ziada iueze nje ya nchi. Alitaka pia izalishe kwa wingi mazao yote ya biashara kama ya pamba, kahawa, chai, mkonge na kakao kwa lengo la kuliingizia Taifa fedha za kigeni.

Sokoine alifanya hivyo akiamini kuwa kilimo ndio uti wa mgongo. Hakutaka Taifa liwe ombaomba ila lenye nguvu kiuchumi. Ndiyo maana alijitahidi kuliwekea msingi imara wa maendeleo kupitia elimu ya kujitegemea na siyo ya kutafuta kuajiriwa.

Hata hotuba yake ya mwisho kwa Taifa aliyoitoa siku moja kabla ya kifo chake alipokuwa akiahirisha kikao cha Bunge mjini Dodoma, Aprili 11, 1984, alisema ni heri mkulima atakayekamatwa akiiba mbolea ili akaitumie vizuri shambani kwake, huyo tutamsamehe, lakini ole wake kiongozi atakayekamatwa kwa kufanya ubadhirifu wa mali ya umma.

Kutokana na kukipa umuhimu wa kilimo, Sokoine ndiye kiongozi wa kwanza aliyetaka mabwana na mabibi kilimo na mifugo wakaishi vijijini karibu na wananchi, kwa msingi huo aliweza kuifanya Tanzania isimame vyema katika dhana ya kilimo kama uti wa mgongo wa Taifa.

Yote haya aliyafanya kwa kujiamini akijua wananchi watatekeleza wajibu wao na Serikali itatekeleza upande wake, kuhakikisha pembejeo zinakuwapo na kupeleka wataalamu wa kutosha vijijini.

Wakati tukiadhimisha miaka 34 ya kifo chake, bado mijadala imeendelea kutoka kwa watu mbalimbali wakilalamika kuwa kilimo kimesahauliwa, asilimia kubwa ya wakulima wameendelea kulima kilimo duni na kwa kutumia zana duni. Wataalamu wanalalamikiwa kutofika vijijini na baadhi yao wameelezwa kuamua kukimbilia kwenye siasa kutafuta masilahi zaidi ya kimaisha.

Ipo haja kwa Serikali kufanya mapinduzi ya kilimo ambayo yatakwenda sambamba na mkakati wa Tanzania ya viwanda kwa kuhakikisha inaweka mazingira yatakayowavutia watu wengi kuingia katika sekta hiyo, ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo maalumu ya kuendesha shughuli za kilimo biashara na kupeleka miundombinu yote muhimu.

Jambo lililo wazi hivi sasa ni kwamba wakulima wana matatizo mengi ikiwamo uhaba wa wataalamu, ufinyu wa masoko ya mazao yao na hasa suala la bei ndogo ya mazao mambo ambayo yamewafanya wengi wao kuendelea kuwa maskini.

Wapo wafanyabiashara wanaokwenda kununua mazao kwa wakulima kwa hila, kuna mifano mingi ya namna mkulima wanavyodhulumiwa kama vile matumizi ya ‘lumbesa’ na ‘kuchumbiwa’ mazao shambani kama vile mkungu wa ndizi na mahindi.

Rai yetu kwa viongozi wa Serikali, watunga sera na wanasiasa, tumuenzi hayati Sokoine kwa kutatua kero za wakulima ili waweze kulima kitaalamu na kwa faida.

Kwa kuwa tunaamini kuwa kilimo ni uhai, basi tukifanye kiwe sehemu ya maisha yetu.