In Summary

Mchele uliopo nchini kwa sasa ni zaidi ya tani milioni 2.2, kiwango kilichotokana na wakulima wa mpunga kupatiwa mbinu bora za kitaalamu.

Moshi. Serikali imesitisha uagizwaji wa mchele kutoka nje ya nchi kutokana na uliopo nchini kutosheleza mahitaji.

Mchele uliopo nchini kwa sasa ni zaidi ya tani milioni 2.2, kiwango kilichotokana na wakulima wa mpunga kupatiwa mbinu bora za kitaalamu.

Katibu mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mathew Mtigumwe alisema jana kuwa mahitaji ya mchele yanatosheleza kwa sasa.

Mtigumwe alisema hayo wakati akizungumza na wakulima wa mpunga kutoka mikoa mbalimbali nchini katika mafunzo yaliyofanyika mjini Moshi yaliyofadhiliwa na Shirika la Misaada la Japan (Jica).

Alisema mahitaji ya mchele nchini ni tani 900,000 na kwamba uzalishaji kwa sasa umeongezeka na nchi ina ziada ya zaidi ya tani milioni 1.2.

“Serikali mwaka huu haina haja ya kuagiza mchele kutoka nje ya nchi, ” alisema Mtigumwe

Alisema wanatambua mchango wa kuwasaidia wakulima unaofanywa na Jica ambapo wale wadogo wa mpunga wamefanikiwa kuongeza kiwango cha uzalishaji tofauti na siku za nyuma.

“Kutokana na uzalishaji huu umeifanya Tanzania kuwa nchi ya tano Kusini mwa Jangwa la Sahara katika uzalishaji wa mpunga baada ya nchi ya Nigeria, Madagascar, Mali na Guinea.”

Mwakilishi mkuu wa Jica nchini, Toshio Nagase alisema zaidi ya wakulima 15,000 wamenufaika na mradi huo na kuweza kujikwamua na umaskini.

Wakulima wanasemaje?

Hadija Hassan ambaye ni mnufaika wa mafunzo hayo, alisema amefanikiwa kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mpunga kutoka magunia matatu kwa eka moja hadi magunia 56.

“Sasa hivi tunakabiliwa na ukosefu wa masoko, hivyo tunaiomba Serikali iangalie uwezekano wa kutupatia masoko ya uhakika ili tuendelee kunufaika na kilimo hiki kwani tumeweza kupeleka watoto shule kwa kupitia kilimo,” alisema Hadija.

Mkulima wa Ifakara mkoani Morogoro, Sued Rashid alisema miaka yote mchele unapatikana mwingi, lakini wafanyabiashara wanaupenda sana unaozalishwa Tanzania, hivyo huusafirisha nje kwa mauzo na kuacha watu nchini wakitaabika kwa bei.

“Huku (Ifakara) mchele ndiyo chai ndicho chakula cha mchana na usiku, nashangaa wanaposema siku za nyuma kulikuwa na uhaba. Uzuri mchele wetu unapendwa mno huko nje na ndiko unakopelekwa kuuzwa,” alisema Rashid kwa njia ya simu kutoka wilayani humo.