In Summary

Taarifa ya Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, ilieleza kuwa kata hizo mpya ni Kelamfua ya Wilaya ya Rombo na Kitaya wilayani Nanyamba.

Dar es Salaam. Wakati vyama vya siasa nchini vikiendelea kuteua wawakilishi wao watakaogombea udiwani na ubunge katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Agosti 12, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kata mbili mpya na kuahirisha uchaguzi katika nyingine nne.

Taarifa ya Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, ilieleza kuwa kata hizo mpya ni Kelamfua ya Wilaya ya Rombo na Kitaya wilayani Nanyamba.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 13 (1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa aliitaarifu tume kuhusu uwepo wa nafasi wazi za madiwani katika Kata ya Kelamfua na Kata ya Kitaya iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nanyamba,” alisema Jaji Kaijage.

Alisema nafasi zote za udiwani zimetokana na kujiuzulu kwa madiwani waliokuwa wamechaguliwa awali. Kadhalika, Jaji Kaijage alitangaza kuahirishwa kwa mchakato wa uteuzi wa wagombea kwenye kata nne za Tindabuligi, Kisesa, Katumba na Mlimba.

Mabadiliko hayo yanafanya jumla ya kata zenye uchaguzi kubaki 77 badala ya 79 zilizotangazwa awali.

Alisema tume itatangaza baadaye tarehe nyingine za uteuzi na uchaguzi katika kata hizo.

Hata hivyo, taarifa ya NEC haikueleza kwa nini mchakato wa uteuzi katika kata nne umeahirishwa.

Akizungumza na wanahabari juzi, Jaji Kaijage alisema uteuzi wa wagombea udiwani utafanyika Julai 16 na kampeni zitaanza Julai 17 hadi Agosti 11, na kwamba siku ya upigaji kura itakuwa Agosti 12.

Jaji Kaijage alivialika vyama vya siasa, wadau wa uchaguzi na wananchi kushiriki uchaguzi huo.

Kura za maoni

Wakati huohuo, diwani wa Chadema aliyejiuzulu na kujiunga CCM, Michael Kunani amebwagwa katika kura za maoni ndani ya CCM katika Kata ya Ikoma Wilaya ya Serengeti mkoani Mara kwa akizidiwa kura moja na Moses Nguhecha.

Kunani na diwani wa Manchira, Joseph Mongita walijiengua Chadema na kuhamia CCM wakiacha nafasi zao wazi. Hata hivyo Mongita hakujitokeza kuchukua fomu.

Katika kura za maoni Kata ya Ikoma aliyeongoza ni Moses Nguhecha (18) akifuatiwa na Kunani (17) huku Mgosi Gaugeri akiambulia kura moja.

Kadhalika, Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kitashiriki kikamilifu uchaguzi wa madiwani na ubunge.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano, Ado Shaibu alisema wameunda kamati maalumu ya mashauriano itakayoongozwa na Omary Shaibu Shaaban ili kushauriana na vyama vingine juu ya kusimamisha mgombea mmoja kwenye maeneo ya kimkakati.

Tayari Kamati Kuu ya CCM imemtangaza Christopher Chiza kugombea ubunge katika Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma. Jimbo hilo awali lilikuwa likiwakilishwa na Kasuku Bilago wa Chadema aliyefariki dunia Mei 26 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa.