In Summary
  • Wananchi wametakiwa kwenda Mahakamani wanapoona haki zao za kutoa maoni zinakandamizwa na watu wengine.

Dar es Salaam. Wakili na mwanaharakati wa haki za binadamu, Jebra Kambole amewataka wananchi kutochoka kwenda Mahakamani pale wanapoona wameonewa na watu au Taasisi za Serikali.

Kambole ameyasema hayo leo Jumanne Juni 25, 2019 wakati wa mjadala kuhusu ushiriki wa wananchi kwenye uongozi wa nchi ambao umewakutanisha wadau mbalimbali.

Kambole amesema zipo sheria nyingi zinazokandamiza uhuru wa kujieleza.

Amezitaja baadhi ya sheria hizo kuwa ni pamoja na sheria ya makosa ya mtandao, sheria ya makosa ya jinai, sheria ya takwimu na sheria ya vyombo vya habari.

Ametolea mfano kesi anazosimamia za watu mbalimbali wenye akaunti za You Tube ambao wameshtakiwa kwa kuwa na wafuasi (subscribers) 40 bila kuwa wamesajiliwa na TCRA.

“Siku hizi maoni binafsi ni kosa la jinai, unaweza ukakamatwa, ukazuiliwa au ukahojiwa. Ninawashauri msichoke mnapoona mmeonewa, nendeni Mahakamani,” amesema Kambole.