In Summary
  • Mama huyo aitwaye Joyce Ali (35), mkazi wa Mtoni kwa Azizi Ali anatamani bahati hiyo imrudie katika sura nyingine itakayobadili maisha yake.

Dar es Salaam. Unamkumbuka mama muuza matunda aliyeuza mzigo wote kwa Rais John Magufuli juzi, katika geti la kampuni ya Oryx pale bandarini jijini Dar es salaam?

Mama huyo aitwaye Joyce Ali (35), mkazi wa Mtoni kwa Azizi Ali anatamani bahati hiyo imrudie katika sura nyingine itakayobadili maisha yake.

Joyce ameomba kuwezeshwa kwa kupatiwa mtaji utakaomsaidia kuinua biashara yake ili kukabiliana na changamoto ya kipato kidogo anachopata.

Mama huyo alimuuzia matunda Rais Magufuli siku mbili zilizopita, dakika chache kabla ya mkuu huyo wa nchi kuondoka bandarini kupitia geti namba tano.

Akitembea kwa miguu kutoka nje kupitia geti hilo, Rais aliwasalimia wafanyabiashara waliokuwa pembezoni pamoja na madereva waliokusanyika kumsikiliza.

Katika tukio hilo, Joyce alipata mshtuko baada ya Rais Magufuli kusogea kwenye meza yake ya matunda na kuyalipia yote kwa Sh30,000, kisha kula na watu waliokuwapo eneo hilo.

Mwandishi wa Mwananchi aliyemtembelea mjasiriamali huyo katika genge lake la wazi jana, alikuta akiwa ameweka meza ndogo yenye ndizi, mapapai, matango na maparachichi.

Genge hilo linapakana na geti namba tano katika Bandari ya Dar es Salaam, lakini ili ufike itakulazimu upitie Barabara ya Mandela.

“Nashukuru sana kwa Rais kuniunga mkono katika biashara yangu, lakini hali si nzuri. Sijajiunga saccoss (chama cha kuweka na kukopa) wala vicoba kwa kuwa naogopa endapo nikikwama itakuwaje, (ila) nikipata msaada wa kukuza mtaji watoto wangu wasikwame masomo nitashukuru sana,” alisema Joyce ambaye jua na mvua vinamhusu wakati wowote katika eneo hilo.

Mama huyo mwenye sura ya tabasamu wakati wote, alisema licha ya kuuza mzigo wote kwa Rais, maisha yake muda wote yako katika hali ya kubahatisha kutokana na mtaji mdogo usioendana na changamoto zinazomkabili.

Joyce anayeishi bila mume, anapambana ili kuhakikisha watoto wake wawili aliowapata katika uhusiano wake wa awali wanakwenda shule, kulipa kodi ya nyumba na chakula kwa familia.

“Mtaji wangu ni Sh50,000 nalipa ada ya mwanangu wa chekechea, Abel John (4) Sh50,000 kila mwezi pale Kwa Aziz Ali. Mtoto mwingine Ibrahim anasoma kidato cha pili, nalipa kodi ya nyumba Sh40,000 kwa mwezi,” alisema Joyce aliyeanza biashara hiyo miaka mitatu iliyopita kwa mtaji wa Sh20,000.

“Mahitaji ni makubwa kuliko mapato ninayoyapata hapa, kwa kawaida nanunua matunda ya Sh50,000 na biashara imekuwa ngumu kidogo kwa sasa kwa kuwa nauza kwa wastani wa Sh25,000 na Sh30,000, faida inayopatikana ni Sh20,000 ambayo inaishia kwenye mahitaji hayo,” alisema.

Joyce alisema angetamani kuona maisha yanabadilika kupitia bahati pekee ya kuonana na Rais Magufuli, wakicheka pamoja huku akinufaika na kuuza matunda yake yote aliyokuwa nayo.

Alichozungumza Rais

Vyombo vya habari jana viliripoti tukio hilo na mazungumzo yaliyosikika kupitia kipaza sauti.

Jocye alisema hakuwa na taarifa wala kufikiri kwamba Rais Magufuli angeweza kusimama na kununua matunda kwenye mazingira yale.

Alisema tukio hilo ni bahati ambayo hakuwahi kuifikiria katika maisha yake.

“Niliona furaha sana kumuona Rais macho kwa macho, hadi akashika beseni langu la matunda, akaniuliza wewe mtu wa wapi? Nikamwambia mimi natokea Tanga, Lushoto, basi akanitania kwamba ‘ninyi wake zetu,” alisimulia Joyce uso wake ukiwa umejaa tabasamu na kicheko.