In Summary

Maisha ya wasanii wa WCB hayaendi bila kiki na asilimia 100 kiki zao, hupitia kwa mademu wenye majina makubwa mjini.

UNAFUATILIA mtandao wa Instagram wa mastaa wa Kundi la Wafasi Classic Baby ‘WCB? Kama wewe ni mfuasi wao nadhani wala hutapata tabu kuling’amu hili.

Jamaa ni kiboko kwa kusaka kiki. Hata bosi wao, Naseeb Abdul ‘Diamond Plutnumz’ ameshawahi kukiri hadharani kuwa yeye ni bingwa wa kiki. Ulimsikia?

Maisha ya wasanii wa WCB hayaendi bila kiki na asilimia 100 kiki zao, hupitia kwa mademu wenye majina makubwa mjini.

Pindi msanii wa kundi hilo akitoa wimbo mpya, ni lazima kwanza kiki ianza au ifuate baadaye ili kuufanya wimbo wake kupata mashiko kwa haraka. Inawezekana ni mkakati wa kundi, ila mimi na wewe hatujui. Tuwaachie wenyewe.

Kiki hizo mara nyingi huwa zinashtua mashabiki na kuwafanya kwa siku kadhaa wakibaki kumzungumzia msanii husika kwa muda mrefu.

Hata hivyo, zipo nyingine zinaharibu taswira na heshima ya msanii husika, pale inapotua kwenye jamii na kukutana na watu wenye uelewa mpana.

Mwanaspoti linakushushia ushahidi wa kiki za WCB hapa.

Diamond

Baba wa kiki sasa! Huyu ndiye kiboko. Jamaa hafanyi mambo kihasarahasara, anajua kujipanga.

Kwanza katika video za Diamond amekuwa akiwatumia warembo anaotoka nao kimapenzi wanaokuwa kivutio na gumzo kwa mashabiki wake. Hali hii humwongezea mashabiki wa kazi zake.

Mshikaji ana akili ya tofauti katika Bongofleva na ndiye an ayeongoza kwa kuwaimba au kuwashirikisha wapenzi wake kwenye kazi zake.

WEMA SEPETU

Sina haja ya kutumia nguvu nyingi kukukumbusha kuhusu drama zake.

Miss Tanzania huyo wa mwaka 2006, ndiye aliyempandisha Diamond katika viwango vya Bongofleva.

Diamond alishawahi kumtumia Wema kama video queen kwenye wimbo wa Moyo Wangu.

Drama za wawili hao za mara kwa mara zilimfanya Diamond kumwimba Wema kwenye wimbo wake wa Nimpende Nani pale alipochombeza kwa kusema “Na Utuache tulale.”

Kama haitoshi akamtaja hadi mama yake Wema kwenye Wimbo wa Kesho. Ushausikia Wimbo wa Sikomi? Diamond amezungumza historia yake ya mapenzi na Wema na Penniel Mungwila ‘Penny.’

Hamisa Mobetto

Ukichunguza kwa undani unaambiwa Hamisa ndiye wa kwanza kutoka na Diamond kabla ya Wema. Unaweza usiamini hili.

Mwanamitindo huyo maarufu ametawala kwenye video ya Salome na kuzaa matunda ya mtoto Abdul Naseeb ‘Dylan’.

Panda shuka za wawili hawa zinaendelea baada ya kiki ya kumlea mtoto wao na kufikishana mahakamani.

Ghafla Diamond akaingia studio na kutoka na ‘Niache’. Umeshawahi kuyatafakari mashairi ya wimbo huo? Unaweza kudhani Diamond hatakaa na kuzungumza tena na Hamisa Mobetto.

Diamond alichukizwa na kitendo cha Hamissa kuwaita mapaparazi wakati mama yake, Sanura Kasim ‘Bi Sandra’ na dada yake Esma Platnumz walipokwenda kumwangalia hospitali alipojifungua.

Kitu cha ajabu kati ya video zisizokuwa na maadili zilizomfikisha Diamond Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufunzwa maadili, mojawapo ilikuwa kati yake na Hamisa wakiwa kitandani.

Sasa ndio kumechafuka zaidi baada ya kutoka kwa video ya Iyena ya Diamond akiwa na Zari Hassan. Familia inaonekana kumtaka Zari aliyeachana na Diamond huku wakimpiga vijembe Hamisa.

Zari Hassan

Ni mzazi mwenza wa Diamond baada ya wawili hao kupata watoto wawili.

Sasa baada ya kutoka kwa video ya Iyena, inayowaonyesha Diamond na Zari wakiwa kama wanandoa mambo yamekuwa moto.

Hii ni video ya pili ya Zari baada ya ileya Wimbo wa Utanipenda?

Meneja wa Diamond, Babu Tale alitupia picha Instagram akienda Afrika Kusini huku akisema anaenda kusuruhisha ugomvi wa wiwili hao. Baada ya muda akasema alikuwa ameenda huko kuzungumzia kuhusu matunzo ya watoto wao.

Drama zinaendelea baada ya Zari kupokea zawadi za pafyumu kutoka kwa Diamond na kumshukuru katika mtandao wa Snapchat.

Kumbuka haya yote yanakuja kwa sababu ya Wimbo wa Iyena na siyo kitu kingine.

Sasa anataka kusikia kuhusu Diamond na Zari. Drama gani itaendelea. Tusubiri tuone.

Harmonize

Dogo anajua kuimba na staili yake, kama Mondi vile. Yuko vizuri. Akijiongeza kidogo tu anaweza kufika mbali.

Alianza kusikika mwaka 2016 na wimbo uliomtambulisha ni ule wa ‘Aiyola’, ngoma iliyoshika chati hadi alipotoa hit ya pili ‘Bado’ akimshirikisha Diamond.

Ili kukuza jina lake, Harmonize akaanzisha uhusiano wenye drama nyingi na demu wa mjini. Mtoto mwenye ngozi ‘laini’ kutoka Uchagani, Jacqueline Wolper Massawe kutoka Bongo Movie.

Mara ya kwanza wengi hawakuamini. Kwa kuwa walifahamu bosi wake, Diamond alishatoka na demu huyo, hivyo isingekuwa rahisi kwa Harmonize kuanzisha uhusiano naye. Ndipo drama za kupelekana kwa wazazi zikaanza Januari 2017.

Harmonize hakumpeleka Wolper kwa wazazi wake Mtwara? Tena akaenda kupiga shoo ya nguvu kwa mara ya kwanza mkoani kwake humo tangu nyota yake ianza kufuta vumbi pale WCB.

Mitandao ya kijamii ikarusha sana picha za wawili hao. Kwa kuweka mkazo tu, sinema hii ilikuwa inasimamiwa na steringi, Diamond mwenyewe.

Haikuchukua muda mrefu Harmonize akatoka na wimbo wa ‘Sina’ ambao ulitumia kama kiki ya kuonyesha Wolper yuko kimapenzi zaidi kwa Harmonize hata kama dogo hana kitu.

Wakati watu wakiujadili wimbo huo, Juni 2017, Harmonize akatoa wimbo wa ‘Niambie’ ambao ndani yake una jina la Gambe analotumia Wolper kama a.k.a yake. Kama kawa kama dawa, kabla ya wimbo huo kutoka picha na video za wawili hao zikatawala kila mtandao zikiwaonyesha wawili hao wakiwa kimahaba zaidi, nyingine wakiwa kitandani.

Hadi kufikia hapo nani hakuamini kama wawili hao hawakuwa wapenzi?

Utata waibuka

Drama katika mitandao zikaendelea hadi ikafika Wolper na Harmonize kufuta picha katika akaunti zao.

Wolper akaandika maneno ya kuashiria kuachana huko Instagram na watu wakanza kuzungumzia kuachana kwao, ghafla ikaja ngoma mpya ya Harmonize ‘Nishachoka’.

Drama za Harmonize na Wolper hatimaye zikawakifanya kuachana na bifu zito la vita ya kurushiana maneno likaibuka mitandaoni.

Harmonize akadaiwa kumsailiti Wolper kwa kutembea na msichana wa Kizungu, Sarah, lakini vita ikazidi hadi kufikia hatua ya kudhalilishana mitandaoni baada ya Harmonize akataja listi ya wanaume waliotembea na Wolper.

Cha kushangaza, hivi karibuni, Harmonize akatangaza kufanya shoo na akamtaja Wolper kuwa MC wa shoo hiyo, kabla ya Wolper kuibuka na kukanusha vikali kuwa hahusiki na shoo hiyo kwa nde wala te. Acha drama ziendelee.

Rayvanny

Jamaa ni mkali kinoma wa kutunga nyimbo kali ndani ya WCB. Naye ameingia katika orodha ya wanaojinufaisha kupitia kiki za mademu.

Kabla ya kutoa ngoma yake ya ‘Siri ya Nini’ aliyopewa ruhusa ya kuitumia na mwanamuziki mkongwe, Hussein Jumbe alitangaza kuachana na mzazi mwenziwe Fahyma.

Watu wakaanza kumwonea huruma demu huyo, kazaa na Rayvanny kisha kaachwa. Ilihuzunisha kwa kweli.

Stori Instagram na mitandao mingine Rayvanny kamtema mama wa mtoto wake, Fahyma.

Ilichukua wiki moja kutangaza kurudiana kwa wawili hao, huku wakianza kupostiana kwenye Instagram. Ghafla ngoma ya Siri ya Nini ikatoka, kitu cha ajabu Video Queen wa ngoma hiyo akawa ni Fahyma. Acha drama ziendelee.