In Summary

Uamuzi huo umetolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shahidi wakati shauri hilo lilipofikishwa kwa ajili ya ushahidi.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetenga siku tatu mfululizo kusikiliza ushahidi wa kesi ya kusambaza dawa bandia za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARVs), inayomkabili aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida na wenzake watano.

Uamuzi huo umetolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shahidi wakati shauri hilo lilipofikishwa kwa ajili ya ushahidi.

Hakimu Shahidi alisema kwamba kesi hiyo itasikilizwa kuanzia Julai 9 hadi 11, mwaka huu.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hilla alidai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya ushahidi, lakini upande wa mashtaka hawakuwa na mawasiliano na shahidi husika.

Tayari mashahidi watatu wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.

Mbali na Madabida, ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Limited cha Dar es Salaam (TPI), washtakiwa wengine ni Mkurugenzi wa Operesheni, Seif Shamte, Meneja Masoko, Simon Msofe na Mhasibu Msaidizi, Fatma Shango, wote kutoka TPI.

Wengine ni Sadick Materu ambaye ni Meneja Udhibiti Ubora wa dawa na Evans Mwemezi ambaye ni Ofisa Udhibiti Ubora wa Dawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kusambaza dawa bandia na kuisababisha Serikali hasara ya Sh148.3 milioni.