In Summary
  • Akizungumza na MCL Digital, Jaydee amesema amefanya hivyo baada ya kuambiwa kuwa ni moja ya sababu inayochangia mtu kuwa na hasira.

Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Judith Wambura maarufu Lady Jaydee amesema amelazimika kuacha kula nyama nyekundu ili kudhibiti hasira.

Akizungumza na MCL Digital, Jaydee amesema amefanya hivyo baada ya kuambiwa kuwa ni moja ya sababu inayochangia mtu kuwa na hasira.

Amekiri tangu achukue uamuzi huo miaka 10 iliyopita anaona kuna mabadiliko kwa kuwa alikuwa ni mtu ambaye hawezi kuzuia hasira zake anapochokozwa.

“Ni kweli mimi ni mtu ninayekasirika haraka. Kudhibiti hali hiyo kwanza nikaacha kula nyama nyekundu miaka 10 iliyopita. Pia, napendelea kukaa sehemu peke yangu mpaka hapo zinapoisha ili kuepuka kufanya jambo baya ambalo naweza kulijutia baadaye,” amesema.

Mbali na mbinu hizo, anasema hapendi kwenda maeneo ambayo anajua yanaweza kumkwaza.

Hata hivyo, anakiri kushindwa kuhimili kuzuia kuwajibu watu wanaojifanya kumjua.

Katika hilo anawasihi mashabiki kutambua kuwa naye ni binadamu, kuna mambo ambayo huwa yanamkwaza na kushindwa kuzuia kuonyesha hasira.