In Summary
  • Hii husaidia kupata takwimu sahihi na kufanya tathmini kabla ya kuanza kwa utekelezaji wake. Katika utekelezaji wake, wananchi husika hushirikishwa ingawa kuna changamoto kutokana na imani zao.

Miradi ya maendeleo inayojumuisha ujenzi wa miundombinu ya zahanati, barabara, kilimo na ufugaji, maji na shule za msingi au sekondari huhusisha utafiti wa muda mfupi kabla ya kutekelezwa.

Hii husaidia kupata takwimu sahihi na kufanya tathmini kabla ya kuanza kwa utekelezaji wake. Katika utekelezaji wake, wananchi husika hushirikishwa ingawa kuna changamoto kutokana na imani zao.

Maendeleao inayotekelezwa vijijini inaweza kukwamishwa na wananchi bila kujali fedha nyingi zinazotolewa na wafadhali au Serikali kutokana na mtazamo tofauti walionao.

Vyombo vya habari wiki iliyopita viliripoti kukwama kwa baadhi ya miradi ya maendeleo wilayani Misungwi kutokana na imani za kishirikina, tukio lililotokea Mkoa wa Mwanza.

Oktoba 2016, watafiti wawili na dereva mmoja wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian (Sari) cha jijini Arusha waliuawa na miili yao kuchomwa moto katika Kijiji cha Iringa-Mvumi kilichopo Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Watafiti hao waliokuwa wakifanya utafiti wa udongo waliuawa baada ya kuhisiwa kuwa ni wanyonya damu.

Matukio haya mawili ni mfano tu wa mengi yaliyogharimu maisha ya watafiti na kukwamisha malengo ya miradi ya maendeleo maeneo mengi nchini.

Suala la kukosa ushirikiano kwa viongozi wa Serikali za Mitaa huko vijijini na baadhi ya mitaa ya mjini pindi watafiti au wakadnarasi wanaporipoti kwenye ofisi hizo kwa ajili ya utambulisho ni kati ya sababu za kushamiri kwa matukio haya.

Maeneo mengine, wananchi hawawatambui maofisa wanaotekeleza miradi ya maendeleo iwe mjini hata vijijini licha ya kupata kibali cha mtendaji au mwenyekiti wa kijiji husika ambaye ameridhia kutoa ushiriano.

Wananchi hawa huwa na maoni tofauti wanapoona mgeni kaingia kwenye mtaa wao au kijijini, wengine huwaza kama ni msaada unaoweza kuwasaidia moja kwa moja kwenye kaya zao lakini wanaokosa matumaini juu ya kupata chochote.

Ikumbukwe, asilimia kubwa ya wananchi wa vijijini ni wana kipato cha chini na wanaishi katika mazingira magumu hivyo kuchangia kukosa uelewa wa kawaida juu ya miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Huko, wanapatikana hata waliokosa elimu ya msingi, hawajui kusoma wala kuandika na kwa kifupi, hawana uelewa wowote wa utendaji wa Serikali ya kijiji au mtaa.

Waliosimamia mradi wa kupunguza umasikini wa Tasaf walishuhudia mengi kutoka kwa walengwa waliokuwa na imani tofauti juu ya kilichokuwa kinaendelea.

Baadhi ya familia zilikuwa zinajifungia ndani ili kutotoa ushirikiano wakidai kuchoshwa na usumbufu wa maofisa waliokuwa wakiwatembelea wakiwa wameongozana na wajumbe wa Serikali ya mtaa au kijiji husika.

Imani ya wananchi ni kuona maendeleo ya moja kwa moja katika maeneo yao ambayo hupungua pale wanapokosa matunda ya mradi kwa wakati.

Kwa upande mwingine wananchi hujenga imani potofu wakati maofisa wa utafiti au maradi wanapowaomba wajitambulishe kwa majina na kutoa taarifa zao na za kaya walizomo.

Serikali za mtaa zinapaswa kutambua kuwa mashirika binafsi, ya kimataifa na Serikali ni wadau wakubwa wa maendeleo katika vijiji na mitaa hivyo waonyeshe ushirikiano mkubwa katika kuwapokea maofisa husika na kuwaongoza kwenye maeneo yao ya kazi.

Serikali ya mtaa husika inawajibika kuwaelimisha wananchi wake ili kuondoa hofu yoyote au imani potofu au za kishirikina na mawazo hasi juu ya miradi ya maendeleo.

Mwandishi anapatikana kwa namba 0756 409 709 au 0658 409 709.