In Summary
  • ATCL iliondolewa kwenye shirikisho hilo mwaka 2008 baada ya kuelemewa na madeni, lakini sasa imekamilisha masharti ya kurejea upya ili kunufaika na mauzo ya tiketi kwa safari za kimataifa.

Dar es Salaam. Wakati likitarajia kuanza safari za moja kwa moja kwenda jijini Mumbai, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limesema linasubiri kurejeshewa uanachama wake wa Shirikisho la Mashirika ya Ndege Duniani (IATA).

ATCL iliondolewa kwenye shirikisho hilo mwaka 2008 baada ya kuelemewa na madeni, lakini sasa imekamilisha masharti ya kurejea upya ili kunufaika na mauzo ya tiketi kwa safari za kimataifa.

Mkuu wa mawasiliano wa ATCL, Joseph Kagirwa alisema jana kuwa wako katika mchakato wa kupata ithibati ya IATA na kurudishiwa uanachana muda wowote.

“Tumeanza kufuatilia kurudi IATA na kupata cheti cha ithibati. Tunalipa madeni yetu ya nyuma ya shirikisho hilo ili turudi. Wakaguzi wa IATA walikuja kutukagua tangu Juni kwa ajili ya suala la ithibati,” alisema.

Baada ya kukamilika kwa ukaguzi huo, alisema wanasubiri kukamilisha utaratibu kabla ya kupata uanachama.

Kwa uzoefu wake, Kagirwa alisema majibu ya wakaguzi hao yanaweza kuchukua mwaka mmoja kabla shirikisho hilo halijatoa uamuzi wa kuwarudishia uanachama.

“Kuwa mwanachama inakusaidia kupata malipo ya tiketi zako moja kwa moja, lakini cheti cha ithibati kina faida ndani ya IATA hata nje.” ATCL imetangaza kuanza safari za kuelekea India mara tatu kwa wiki. Ndege yake itakuwa inatoka Dar es Salaam kila Jumatano, Ijumaa na Jumapili na kurudi kutoka Mumbai Jumatatu, Alhamisi na Jumamosi.

Kwa safari moja ya kwenda au kurudi, kila abiria wa shirika hilo la umma atalipa Dola 286 za Marekani (zaidi ya Sh643,000) au Dola 455 (zaidi ya Sh1.024 milioni) kwenda na kurudi.

Licha ya shirika hilo kuuza tiketi zake lenyewe, Kagirwa alisema ATCL imesaini mkataba na kampuni mbili za kimataifa wakati wakisubiri kurejea IATA. Alizitaja kuwa ni Hann Air ya Ujerumani na Travel Porto.

Kwa kushirikiana na kampuni hizo, ATCL itaweza kuuza tiketi zake ndani ya IATA kwa kuwa kampuni hizo zimepewa leseni ya kuuza tiketi za mashirika ambayo hayapo ndani ya shirikisho hilo.

ATCL imeanza safari za nje ikiwa na ndege nne; Bombardier Q400 tatu na Boeing 787-8 Dreamliner moja. Baada ya kupata hasara kwa muda mrefu, shirika hilo linatarajia kuanza kujiendesha kwa faida kuanzia 2023 tangu lilipofufuliwa 2016.

Licha ya Mumbai, ATCL inafanya safari za kwenda Comoro, Uganda na Burundi huku kukiwa na mipango ya kwenda China, London Uingereza, Afrika Kusini na magharibi mwa Afrika ndege nyingine za shirika hilo zitakapowasili.

Awali ATCL ilitangaza kuanza safari za Mumbai mwezi huu, lakini ikabadili na sasa itaanza kati ya mwishoni mwa Oktoba au mwanzoni mwa Novemba. Kuhusu mabadiliko hayo, Kagirwa alisema kuna baadhi ya mambo hayajakamilika lakini kila kitu kitakwenda vizuri.

“Matangazo ya nauli tuliyotoa ni ishara kwamba tuna uhakika wa kuanza safari. Tutatangaza lini hasa wateja waanze kununua tiketi,” alisema.

Biashara

Miaka miwili tangu lilipofufuliwa, shirika hilo limeongeza wateja hadi asilimia 24 kutoka asilimia mbili liliokuwa linawahudumia hapo awali.

Kuongezeka kwa wateja hao kuliifanya ATCL kuongeza mapato hadi Sh4.5 bilioni kwa mwezi mwaka 2017 tofauti na mwaka 2016 ilipokuwa inapata Sh700 milioni ndani ya kipindi hicho.

Ufanisi huo umelisaidia shirika hilo kupunguza hasara kutoka Sh14.2 bilioni liliyokuwa linapata mwaka 2016 hadi Sh4.3 bilioni mwaka 2017.

Katika kuboresha biashara ndani na nje ya nchi, ATCL inatarajia kupokea ndege mpya mbili aina ya Airbus A220-300 na Dreamliner nyingine mwaka 2019.

Hata hivyo kurudi IATA kutaisaidia kujiimarisha zaidi kutokana na ushirikiano itakaoupata kutoka mashirika 290 ya ndege wanachama waliokuwapo hadi mwishoni mwa mwaka jana kutoka mataifa 117 duniani. Makao makuu ya IATA yapo nchini Canada.