Mara nyingi katika hatua za awali za tatizo hili dalili huwa hazijitokezi, huanza pale mwili unapoanza kudhurika kutokana na figo kushindwa kufanya kazi yake.

Viashiria na dalili hutokana na uwepo wa mrundikano wa taka sumu na maji mwilini, vitu hivi mwili huitaji kuvitoa kwani vinapobaki husababisha kutokea kwa madhara mbalimbali.

Takasumu hizo na mabaki yasiyotakiwa na mwili ndio yanayosababisha mwili kuwa dhaifu, kupumua kwa shida, kulegea sana na kuchanganyikiwa.

Kushindwa kuondolewa au kuchujwa katika mzunguko wa damu kwa madini ya Potasiamu ndiyo chanzo kinachosababisha kuwa na mapigo yasiyo na mpangilio.

Kazi ya figo siyo tu kuchuja takasumu zilizopo katika damu na kuziondoa mwilini bali pia kuweka sawa kiwango cha madini na chumvichumvi, kudhibiti msukumo wa damu na kusisimua mwili kutengeneza chembe hai nyekundu za damu.

Vile vile figo hudhibiti kiwango cha tindikali katika damu, kiwango cha maji mwilini, kuchuja na kuondoa mabaki yaliyotokana na kuvunjwa vunjwa kwa protini na tindikali ya uriki inayotokana na kuvunja vunjwa kwa DNA.

Vitu hivyo baada ya kuvunjwa vunjwa ndivyo vinavyosababisha kupata zao lijulikanalo kitabibu kama Blood Urea Nitrogen (BUN) na Creatinine (CR) ambavyo ndiyo hata watoa huduma za afya hupima kiwango chake katika damu ili kujua utendaji wa figo.

Hapa tunaweza kupata picha ni kwa namna gani kiungo hiki kilivyo nyeti katika miili yetu, endapo utendaji kazi wake utayumba aidha kwa kuvamiwa na magonjwa au kuharibiwa kwa namna yoyote ile inaweza kumwatarisha kupata madhara makubwa yanayoweza pia kusababisha kifo.

Kama tatizo halitabainika na kutibiwa mapema madhara ya figo kushindwa kufanya kazi huweza kujitokeza kutokana na kupata ugonjwa sugu wa figo. Dalili na viashiria ni pamoja na kuishiwa nguvu na kuwa mdhaifu ghafla na kwa haraka, mwili kuwa mlegevu, kupumua kwa shida au pumzi kukata na kutopata kabisa haja ndogo kwa zaidi ya saa 24-72 hata baada ya kunywa maji au kuwekewa maji kwa njia ya mshipa. Mwandishi wa makala haya ni daktari wa binadamu