Wazia unaamka asubuhi na kuhisi maumivu kutoka sehemu mbalimbali za mwili wako yakiambatana na uchovu.

Huenda maumivu hayo yanatokana na kuhudhuria shughuli zako la kila siku, unashindwa kwenda hospitali kumuona daktari kwa ajili ya ushauri, unaamua kwenda duka la dawa la karibu kununua dawa za kutuliza homa na maumivu, unakunywa na zinaonekana kukusaidia.

Lakini baada ya saa moja au siku kadhaa, hali ile inarudi tena, unaamua kufanya vilevile.

Ukweli ni kwamba, huu ni mwenendo wa watu wengi, lakini je umeshawahi kujiuliza kuwa kutumia dawa bila kupata ushauri sababu tu siku za nyuma ilikusaidia ni makosa kiafya?

Naomba nikukumbushe msomaji, dawa siyo kitu cha haraka sana kukifikiria hasa kama tatizo lako la kiafya siyo la dharura. Siku moja nilikutana na John (sio jina halisi), kwenye hospitali ninayofanya kazi, mwenye miaka takribani 40 hivi. Mgonjwa huyu alikuwa akilalamika maumivu ya kichwa na uchovu kwa zaidi ya wiki mbili hivi.

Kwa kifupi hali hii ilisababisha John ahisi homa na ilipofika tu zamu yake ya kuingia katika chumba cha daktari kabla ya yote alianza kwa kuniambia: “Daktari katika dawa utakazonipa tafadhali usisahau za malaria na za maumivu, hii hali imenitesa kwa zaidi ya wiki mbili ni lazima itakuwa ni malaria.”

Baada ya kumaliza kujielezea vizuri kuhusiana na kile anachokipitia, ikabidi nimuulize maswali machache ili kubaini chanzo cha maumivu ya kichwa na uchovu anaoupata. Kutokana na majibu yake, nilijua huenda hana homa, lakini alikuwa anahimiza zaidi nimpime malaria ili nimpe dawa za malaria.

Kutokana na maelezo yake, mgonjwa alionekana kutokuwa sawa kisaikolojia kwasababu ya matatizo kadhaa aliyokutana nayo na kumuacha kwenye msongo wa mawazo. Ni dhahiri maumivu ya kichwa na uchovu yalitokana na sababu za kisaikolojia na mwili kukosa kiwango cha kutosha cha maji.

John, sikumpima malaria kama alivyotarajia, badala yake nilimshauri kurudisha furaha yake na kuwa sawa kisaikolojia na kuhakikisha anakula chakula na kunywa maji ya kutosha na kuhakikisha anapata muda wa kupumzika.

Siku chache baadaye, John alirudi kunipa mrejesho na kunishukuru kwa ushauri niliompa.

Mwandishi wa makala haya ni daktari kutoka hospitali ya TMJ SUPER SPECIALIZED POLY-CLINIC.