Hali yako kiafya siyo nzuri na unahisi una malaria kutokana na kuwa na dalili zote za ugonjwa huo.

Unaamua kwenda zahanati kupata vipimo vya afya, unakutana na foleni ya wagonjwa, hivyo unafuata utaratibu wa kwenda kumuona daktari kisha unachukuliwa vipimo na kupelekwa maabara.

Ndani ya saa moja, ukiwa umekaa kwenye benchi huku umeshika tama, anakuja muuguzi kukuita ili uende kuchukua majibu yako kwa daktari ambayo yanaonyesha una maambukizi ya njia ya mkojo (UTI).

Hakika ugonjwa huu umekuwa ‘maarufu’ siku hizi kwa kuwa wengi wanaokwenda katika baadhi za hospitali, zahanati au vituo cha afya kupata tiba huambiwa wana UTI.

Huenda hiyo ndiyo sababu ya kushamiri kwa biashara ya kuuza dawa za ugonjwa huo kwenye baadhi ya zahanati na vituo vya afya.

Utafiti uliochapishwa miaka kadhaa iliyopita na Asina Pacific Journal of Tropical Medicine, umeonyesha kuwa zahanati na vituo vya afya binafsi hulenga kuuza dawa kama chanzo cha mapato badala ya kuangalia afya ya mteja(mgonjwa).

Kwa mujibu wa utafiti huo, vituo vya afya na zahanati binafsi huongeza malipo kwa mgonjwa kwa kumuandikia sindano za ugonjwa huo.

Wagonjwa wasemaje?

Wagonjwa saba kati ya 10 waliohojiwa na gazeti hili kwenye vituo vya afya viwili na zahanati sita waliopimwa afya kutokana na kusumbuliwa na homa, waliambiwa vipimo vyao vimeonyesha wana UTI.

“Hee huu ugonjwa umening’ang’ania kila nikijisikia vibaya nikipima nakutwa na UTI na dawa ninazopewa ni hizi hizi Ciprofloxacin,”anasema Zulfa Zayd ambaye ni miongoni mwa wagonjwa waliohojiwa na gazeti hili. Nilihama zahanati na huku nako nimekutana na yale yale, kilichobadilika ni aina ya dawa huku nimepewa Ciplo, nimechoka jamani.”

Agness Shao aliyekuwa akipima afya kwenye zahanati iliyopo maeneo ya Kinondoni anasema anajua ugonjwa wake ni huo.

“Nikijisikia vibaya nakwenda kupima kwa ajili ya kujiridhisha, lakini najua kabisa huu ndiyo ugonjwa wangu kwa sababu tunatumia choo kimoja watu wengi,” anasema Shao.

Wataalamu wa afya wazungumza

Mganga mkuu wa Serikali, Profesa Muhammad Kambi anasema waliopewa mamlaka ya kulinda afya za wananchi wanaonekana kulisahau jukumu lao na kwa kufanya hivyo wanahatarisha maisha ya wananchi.

“Tumekuwa tukisema mara nyingi hatua za kupima maradhi hayo, kwanza unaupima mkojo na unaweza kupata mabadiliko ya mkojo kwa kupima kipimo cha kwanza ukahisi ni UTI, ilihali kitaalamu ni lazima kujiridhisha kabla ya kutoa uamuzi wa majibu kwa mgonjwa,”anasema Profesa Kambi.

Anaongeza kuwa mkojo unapopimwa unaweza kuonyesha kuwa kuna bakteria, ili kujiridhisha kama ni wa ugonjwa huo lazima wale bakteria waoteshwe hatua hiyo kitaalamu inaitwa (culturing bacteria).

“Ili upate majibu sahihi kipimo hiki huchukua saa 48 kwa uchache hadi 72, tofauti na hapo majibu hayo si sawa. Tunakemea kila siku kumpa mtu dawa za ugonjwa asiokuwa nao... ni kumtia usugu, kwa sababu ukifanya na kipimo cha kuotesha bakteria kinakupa na mwelekeo wa dawa gani atumie, kwa kuhisi hisi lazima utampa isiyokuwa sahihi,” anasema Profesa Kambi.

Daktari Godfrey Materu wa Kituo cha Afya cha Arafa kilichopo maeneo ya Temeke Dar es Salaam, anasema kuna wagonjwa wanakwenda kupima wakiwa na majibu yao kichwani.

“Kuna wakati tunalazimika kutoa elimu, kwa sababu wagonjwa huja na majibu ya magonjwa yao kichwani, wanapoambiwa hawana homa wanakasirika na kwenda kupima mahali kwingine.

“Kuna wakati nilinusurika kufukuzwa kazi kwenye zahanati fulani baada ya kumueleza mgonjwa aliyekuwa anapata homa kuwa hana malaria, UTI wala Typhoid badala yake ana uchovu akanywe maji na apumzike muda mrefu, ”anasema Dk Materu.

Anafafanua kuwa mgonjwa alikuwa anamfahamu mwenye zahanati ndipo alikwenda kumwambia kuwa hakupimwa ipasavyo.

“Aliambiwa (na mwenye zahanati) aje siku inayofuata na asilipe; apimwe na daktari mwingine. (alipopimwa) alikutwa na UTI nyingi na malaria wadudu watano na kununua dawa pale pale na aliondoka kwa furaha,”anasema.

Kutokana na vipimo hivyo kutofautina na vyake, bosi wake alimfokea na kumuona kama mtu anayetaka kumfukuzia wateja.

“Sipingani na hilo, lakini nashauri wagonjwa wawaamini wataalamu wa afya, badala ya kuja na majibu ya homa zao kwa madai wanajijua,” anashauri Dk Materu.

Utaratibu wa vipimo vya UTI

Mkuu wa mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha KCMC, Profesa Alfred Mteta anasema ili kujua kama mtu ana UTI au la, mkojo wake unatakiwa kupita kwenye vipimo saba.

Anasema vipimo hivyo vikibainisha kuwapo kwa bakteria ndiyo wataoteshwa kupata uhakika kama ni maradhi hayo au la, na itafanyika kwa saa 48 au 72.

“Kinachofanyika sasa ni biashara badala ya huduma, hawa wenye hizi zahanati wanalenga zaidi kuuza dawa.

“Wanasahau kuwa kazi yao ni kulinda afya za watu na siyo kuwaumiza, kumpa mtu dawa kwa ugonjwa asiokuwa nao ni kuufanya mwili uwe sugu na usikubali matibabu,”anasema.

Profesa Mteta anasema UTI inaanza na dalili kwa mgonjwa ikiwamo kuhisi maumivu au moto kwenye njia ya mkojo na kukojoa mara kwa mara.

“Baada ya dalili hizo mgonjwa akisikilizwa na kupimwa na daktari, hufanyiwa pia vipimo vya maabara. Kipimo cha kwanza na cha muhimu sana ni urinalysis ambacho pamoja na mambo mengine mkojo wa mgonjwa huzungushwa kwenye mashine maalumu (centrifuge) halafu huangaliwa kwenye darubini!,” anasema Profesa Mteta.

Akielezea zaidi anasema lengo ni kuangalia kama kweli kuna ushahidi wa UTI hasa uwapo wa white cells na red cells (Seli nyeupe na nyekundu) nyingi.

“Vilevile huangalia uwapo wa bakteria katika mkojo pamoja na aina nyingine za seli na vijidudu,” anasema.

Akizungumzia hatua ya pili, anasema ni kuufanyia ule mkojo ‘culture’ yaani kuotesha na kutambua aina ya vidudu vilivyo kwenye mkojo.

“Hii ya culture huendana na sensitivity test yaani vile vidudu vilivyoota hujaribiwa kwenye maabara ni dawa gani itafaa kuvitibu. Hatua zote hizi zinachukua saa 48 hadi 72! Lakini zinampa daktari uhakika wa uwapo wa UTI na matibabu gani yatolewe yaani antibiotic gani na kwa dose gani na muda gani.

“Huo ndiyo utaratibu ambao sasa unavunjwa na baadhi ya watu wasio na weledi kwenye taaluma ya afya ambao huchukua njia ya mkato na kubambikiza wateja UTI ili kuwauzia dawa tu,” anasema Profesa Mteta. Pia, anasema wagonjwa wanaweza kuathirika na antibiotics hizo na vilevile dawa holela husababisha usugu wa vijidudu kwa antibiotics.