In Summary
  • Harakati za kuanza masomo zilijidhihirisha si katika shule tu, bali hata katika maeneo mbalimbali ambako makundi ya wanafunzi waliokosekana kwa muda wa takriban mwezi mzima, jana walionekana mitaani wakienda au kutoka shuleni.

Jana ilikuwa mwanzo wa muhula mpya wa masomo wa mwaka 2019 kwa shule zilizo nyingi za msingi pamoja na zile za sekondari.

Harakati za kuanza masomo zilijidhihirisha si katika shule tu, bali hata katika maeneo mbalimbali ambako makundi ya wanafunzi waliokosekana kwa muda wa takriban mwezi mzima, jana walionekana mitaani wakienda au kutoka shuleni.

Katika hali ya kawaida mwanzo mpya au mwaka mpya wa masomo unatarajia kuwa na mengi mapya hasa ukizingatia kwamba makosa yaliyopita yanakuwa yamefanyiwa kazi.

Pamoja na juhudi kubwa ambazo Serikali imezifanya katika sekta ya elimu ikiwamo kuziboresha na kuzipa hadhi shule za Serikali ambazo zilikuwa katika mazingira yasiyoridhisha, bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika elimu.

Wakati muhula mpya wa masomo ukianza, mkoani Arusha umeripotiwa utaratibu mpya wa wanafunzi kusoma kwa zamu katika shule moja.

Utaratibu huo wa dharura umetokana na wanafunzi waliofaulu kuwa wengi wakati vyumba vya madarasa kwa ajili yao ni vichache.

Takwimu zinaonyesha kuwa wanafunzi waliofaulu kuanza kidato cha kwanza mwaka 2019 kwa mkoa huo ni 33,035, kati yao 18,716 ambao ni zaidi ya nusu hawakupangiwa shule kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Kutokana na tatizo hilo, viongozi mkoani Arusha waliamua kuchukua hatua ya dharura kwa wanafunzi hao kusoma kwa zamu kwa kipindi cha miezi mitatu wakati ujenzi wa maradasa ukiendelea.

Imeahidiwa kwamba hadi Aprili ujenzi wa madarasa utakuwa umekamilika na hivyo wanafunzi watapata nafasi ya kusoma katika hali ya utulivu badala ya kuchoshana kwa kupeana zamu.

Ni imani yetu kwamba ujenzi wa madarasa utafanywa kikamilifu na kuhakikisha unakamilika katika muda uliopangwa na isiwe kwa Arusha tu bali kote Tanzania.

Ni vyema mikoa yenye changamoto za vyumba vya maradasa ichukue hatua za dharura kama Arusha walivyofanya, lakini pia ijiwekee malengo ya kutatua changamoto hiyo.

Zaidi ya hilo tungependa pia kukumbusha kuwa changamoto ya vyumba vya madarasa ni moja ambayo katika hali ya kawaida inaambatana na nyingine mfano madawati, matundu ya vyoo pamoja na walimu.

Kwa hali hiyo tungependa kuona inapotatuliwa changamoto ya madarasa ifikiriwe pia ile ya matundu ya vyoo, lakini pia yasijengwe madarasa tu halafu suala la madawati likaachwa kuwa mtihani mwingine.

Wahusika pia wasisahau changamoto ya walimu, madarasa yatakapoongezwa maana yake na walimu wa kutosha watahitajika. Haya yote ni mambo ambayo yanakwenda sambamba na yote yanatakiwa kupewa uzito unaostahili.

Tutakuwa wa kwanza kusikitika iwapo vyumba vya madarasa vitakamilika, tena vya kutosha, lakini kukawa na changamoto ya madawati, walimu pamoja na matundu ya vyoo. Haya yote ni muhimu yaangaliwe kwa upana na wahusika.