In Summary
  • Nashawishika kutaka kufahamu ni kwa muda gani sasa anawauguza watoto wake wodini hapo. Lakini ninachostaajabu zaidi, baba huyu anawauguza watoto wake watatu aliozaa na mkewe, Mnchari Maro (45) kwa muda mrefu hospitalini hapo.

Wakati nikifuatilia taarifa za matibabu kwenye Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (Moi), ninakutana na baba mwenye watoto wawili anayeonekana kuwahudumia kwa moyo, ndani ya wodi ambayo wanaouguza watoto waliolazwa ni wanawake pekee.

Nashawishika kutaka kufahamu ni kwa muda gani sasa anawauguza watoto wake wodini hapo. Lakini ninachostaajabu zaidi, baba huyu anawauguza watoto wake watatu aliozaa na mkewe, Mnchari Maro (45) kwa muda mrefu hospitalini hapo.

Maro Mwirabi (57) amejitoa kwa ajili ya maisha ya watoto wake, si jambo la kawaida kwani kwa zaidi ya miaka 10 sasa anaishi wodini hapo. Huwaandalia chakula, kuwaogesha na hata kufuatilia matibabu ya watoto wake hao.

Sakata la baba huyu kulea wanawe wodini kwa kipindi chote hicho, limetokana na tatizo la ulemavu wa miguu ‘Club Foot’ maarufu miguu vifundo linaloikumba familia yake.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Maro ambaye ni mkazi wa Nyiboko Kata ya Kisaka Wilayani Serengeti Mkoa wa Mara, anasema mke wake alianza kujifungua watoto wenye tatizo hilo mwaka 1997 katika uzao wake wa tatu.

“Niijaribu kutafuta tiba Bugando lakini ilikuwa ngumu, wakati huo waliozaliwa walikuwa ni Mwirabi Marwa na Moga Marwa ambaye alikuwa na miaka miwili na huyu mwirabi alikuwa mkubwa miaka zaidi ya 9.”

Anasema mwaka 2008 aliamua kutafuta tiba Moi na watoto hao walitibiwa na mkubwa alipona kabisa, na sasa ana miaka 19.

“Yeye alishapona kabisa na miguu ilinyooka lakini kutokana na kuhangaikia tiba hakufanikiwa kwenda shule.”

Anasimulia zaidi, “Hawa watoto niliwazaa kwa awamu, mkubwa alikuwa na tatizo la nyayo kutokanayaga chini na huyu wa pili pia alikuwa na tatizo hilohilo, wakati huo Bhoke alikuwa hajazaliwa, mwaka 2012 mke wangu akapata mimba nyingine akajifungua Bhoke naye akaonekana ana tatizo hilohilo.”

Anasema baada ya kupata taarifa za mkewe kujifungua mtoto mwenye tatizo la miguu vifundo alirudi nyumbani na kumchukua mtoto huyo akiwa na miaka miwili ili apate tiba mapema na baada ya upasuaji binti huyo wa miaka mitano sasa amepona.

INAENDELEA UK.18

Hata hivyo Maro anasema kwa kipindi chote ambacho amekuwa akiuguza watoto wake, amekuwa akipewa mahitaji yote muhimu na hospitali hiyo ikiwamo chakula, malazi na mavazi kupitia ofisi ya Ustawi wa Jamii.

Moi yaeleza ilivyowatibu

Mkurugenzi wa Tiba wa Moi ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji, Samuel Swai anasema mguu kifundo ni tatizo linalojitokeza kwa mtoto tangu anazaliwa, huwa anazaliwa akiwa na mguu usio wa kawaida, unakuwa una kifundo au kitu kama kirungu.

Anasema sababu zinazosababisha tatizo hilo bado hazijulikani lakini watoto wawili kati ya 100,000 wanaozaliwa hukutwa na tatizo hilo.

Dk Swai anasema hilo ni tatizo la kibaolojia ambalo hutokea sehemu tofauti duniani lipo zaidi maeneo ya Mashariki ya mbali na Afrika, lakini Ulaya na Marekani halionekani sana.

“Ni tatizo la kurithi na haijulikani linaanzia wapi na linakuwa na vinasaba linakwenda kwenye familia wazazi wanakuwa na vinasaba na inafanya mtoto anazaliwa hivyo, misuli yake hailegei sawa na watoto wengine, inakuwa migumu na husababisha miguu inapinda na kuwa kama ina kifundo au kirungu. Mtoto hukanyagia sehemu ya juu badala ya kukanyagia unyayo,” anasema.

Akimwelezea baba Bhoke, Dk Swai anasema kwa bahati mbaya watoto wake wote watatu waliozaliwa kwa umri tofauti walikuwa na tatizo hilo lakini Moi ilihakikisha inatoa tiba kwa ajili yao.

“Huyu mmoja kwa mara ya kwanza alipokuja takribani miaka 10 iliyopita akiwa na mdogo wake, tuliwanyoosha mguu yao kwa kutumia bandeji ngumu (POP) na tuliwatengenezea viatu, huyu mwingine hakupona kabisa ila tulifanikiwa kunyoosha miguu ya huyu mmoja, wakati anaendelea na tiba mdogo wake naye akazaliwa akiwa na tatizo hilo,” anasema Dk Swai.

Kwanini baba Bhoke anaendelea kuishi Moi

Dk Swai anasema familia hiyo inyanyapaliwa na jamii ya kijijini alikotoka.

“Watu wamejenga imani za kishirikina, wana mfukuza kijijini wanasema eti atawapelekea mkosi, wanadai mtoto akizaliwa na ulemavu huo ni laana, kwa hiyo ili isiwapate na wengine, inabidi wasionekane kijijini hapo,” anasema Dk Swai.

Anasema licha ya watoto hao kutibiwa na kupona, lakini baba yao anahofia kurejea kijijini kwao kwamba wanaweza kumdhuru.

“Lakini huenda siku moja atarejea kwasababu baada ya Moi kumtibu yule mtoto mkubwa na miguu yake kunyooka kabisa, ile kasi ya watu wa kijijini kutaka kumdhuru imepungua,” anasema daktari huyo.

Hatua zilizochukuliwa na Moi baada ya matibabu ya watoto

Dk Swai anasema wakati mtoto mmoja akiendelea na matibabu hospitalini hapo, Moi iliwasiliana na maofisa wa ofisi ya ustawi wa jamii baada ya kubaini mzazi wao hana uwezo wa kuwahudumia.

Nayo ikaamua kutoa sehemu ya kumhifadhi mzee huyo kwa kumpatia vitanda, matibabu na chakula. Pia inawapatia dawa bure na mavazi.

“Kati ya wagonjwa wengi tuliowatibu kwa muda watoto wa huyu mzee ni miongoni na kupitia ustawi wa jamii tunawasaidia sana,” anasema Dk Swain a kuongeza:

“Kwa sasa tunapambana watoto waende shule na yeye arudi akaendelee na maisha yake.”

“Clup foot linatibika si tatizo la kurogwa na kama mtoto atawahishwa hospitali na kuanza matibabu hawezi hata kufanyiwa upasuaji, atakuwa akinyooshwa kila siku na baadaye anapatiwa matiba ya kutengenezewa kiatu, akifikisha miaka mitatu anakuwa analala nacho,” anasema Swai.

Anasema zaidi ya asilimia 80 ya watoto wanaozaliwa kutokana na miguu vifundo wanapona.

Licha ya kuwapo wachache ambao hutibiwa na tatizo likajirudia tena.

Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Dk Respicious Boniface anasema taasisi yake inatibu maradhi yote ya mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu kuanzia watoto wadogo hadi watu wazima.

Anasema tiba ya miguu vifundo imekuwa ikitolewa katika taasisi hiyo kwa watoto wengi ambao hufika miguu ikiwa imepinda na pindi wanapotibiwa, zaidi ya asilimia 80 hupona kabisa.

“Nitoe wito, wanapopata mtoto mwenye tatizo hili wafike Moi haraka mtot akiwa bado mchanga, kwasababu wapo wanaodhani kwamba mtoto miguu yake ikipinda atakuwa mchezaji mzuri wa mpira au anakuwa na kipaji fulani cha michezo, siyo kweli. Hii si tiba mpya ipo tangu taasisi hii iliponzishwa tulikuwa tunaiita Clup foot, mpaka sasa tumeshawatibu watoto zaidi ya 20,000,” anasema.

Dk Boniface anataja takwimu za miezi mitatu za watoto waliolazwa kwa ajili ya kupatiwa matibau hayo hospitalini hapo kuwa Oktoba walikuwa watoto 66, Novemba 64 na Desemba ni 80 na waliofanyiwa upasuaji ni watoto 156.