In Summary
  • Katika uhakiki huo watumishi zaidi ya 9,000 walibainika kutokuwa na vyeti halali jambo lililosababisha idara ya utumishi kusitisha ajira zao.

Tangu mwaka 2016 Serikali ilipositisha ajira za watumishi wa kada mbalimbali kwenye taasisi za umma zilizotokana na kubainika na vyeti feki, tatizo la upungufu wa watumishi hususan sekta ya afya limekuwa likijitokeza kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Katika uhakiki huo watumishi zaidi ya 9,000 walibainika kutokuwa na vyeti halali jambo lililosababisha idara ya utumishi kusitisha ajira zao.

Kutokana na sababu hiyo, tatizo la watumishi wa sekta ya afya limekuwa kubwa hasa maeneo ya vijijini ambako baadhi ya vituo vimebakiwa na watumishi wasiozidi watatu ambao wanahudumia zaidi ya wagonjwa 400 kwa mwezi au zaidi.

Mathalan, katika Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, tatizo hilo limevikumba vituo vya afya vya Matale na Igongwa vilivyopo katika Kata ya Sumbugu baada ya kubakiwa na watumishi wawili kila kimoja wanaoweza kuhudumia wananchi zaidi ya 20 kwa siku. Kutokana na hali hiyo, wananchi wa maeneo hayo wanasema wanalazimika kutembea umbali wa kilomita 18 kwenda na kurudi katika Kituo cha Afya Misasi kufuata huduma za afya.

Wananchi wengine pia wanasema kutokana na changamoto hiyo wajawazito hulazimika kujifungulia nyumbani huku wagonjwa wengine wakilazimika kutumia dawa za kienyeji.

Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dk John Nyorobi, tatizo la vyeti feki lililowaondoa watumishi 32 wa afya, kati ya 69 walioondolewa wilayani humo limesababisha kuwapo kwa upungufu mkubwa wa watumishi wa ngazi hiyo hususan katika maeneo ya vijijini. Halmashauri hiyo ina jumla ya watumishi 514 huku mahitaji yakiwa ni watumishi 1,028.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Eliud Mwaiteleke anasema Serikali tayari imeanza kuajiri watumishi wengine wa idara ya afya na kwamba itaanza kuwahamisha wengine waliopo kwenye vituo vya mjini kwenda vijijini ambako kuna tatizo kubwa.

Pamoja na kudai kuwa zipo changamoto zinazowakabili washindwe kuwahamisha watumishi likiwemo suala la kukosa fedha za uhamisho, lakini watajitahidi kuwahamisha angalau watumishi wawili ili wakasaidie katika vituo hivyo.

Wakati halmashauri hiyo ikikabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi hao, takwimu zinaonyesha kuwa kuanzia Januari mwaka jana hadi Oktoba, vifo 17 sawa na asilimia 27 ya vifo vyote 63 wilayani Misungwi kwa watoto chini ya miaka mitano, vilitokea.

Kadhalika, vifo vya watoto wachanga tisa sawa na asilimia tisa ya vifo vyote 55 wilayani humo vilitokea, huku vifo vya wajawazito vikiwa ni vitatu ambavyo ni sawa na asilimia 30 ya vifo vyote 10 wilayani humo.

Ingawa hakuna uhusiano wa moja kwa moja, upo uwezekano wa upungufu wa watumishi wa afya kuchangia hali hiyo.

Pamoja na Serikali kutangaza kuanza kuajiri watumishi wapya, ni vyema ikazingatia zaidi kwenye maeneo ya vijijini ambako ndiko kuna tatizo kubwa la upungufu wa watumishi wa afya.

Vilevile maeneo hayo bado yanahitaji elimu ya umuhimu wa wananchi kwenda hospitali kutibiwa kuliko kutumia dawa za asili ambazo zingine zinasawababishia madhara, kwani katika baadhi ya meneo bado lipo tatizo la imani potofu juu ya matumizi ya dawa za hospitali kuwa hazitibu, hivyo wengi wao hukimbilia kwa waganga wa kienyeji. Vilevile Serikali kwa kushirikiana na jamii husika ihakikishe inaboresha miundombinu muhimu ili kuwarahisishia watumishi wapya wasitumie muda mrefu kufika sehemu zao za kazi, ikizingatiwa kwamba lipo tatizo la watumishi kukimbia vituo vyao vya kazi kutokana na kukosa huduma muhimu kwa visingizio mbalimbali. 0757 708 277