In Summary
  • Kwa mara ya kwanza tangu yalipoanzishwa zaidi ya miongo minne iliyopita, yanafanyika kwa siku 16 ili kuwapa nafasi wananchi kupata elimu ya masuala mbalimbali.

Maonyesho ya Sabasaba yasiishe bila kutuachia somo la msingi tutakaloliendeleza siku za usoni kuimarisha baadhi ya mambo muhimu kijamii na kiuchumi.

Kwa mara ya kwanza tangu yalipoanzishwa zaidi ya miongo minne iliyopita, yanafanyika kwa siku 16 ili kuwapa nafasi wananchi kupata elimu ya masuala mbalimbali.

Kati ya mengi ya kujifunza kutoka kwenye maonyesho haya ni shauku ya Watanzania kuviona vivutio walivyo navyo hasa wanyamapori.

Kwenye maadhimisho ya Sikukuu ya Sabasaba, mamia ya wananchi walijitokeza kwenye banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda kuwaona na kupiga picha na wanyama tofauti na wengi wao walivutiwa zaidi na simba.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye vivutio vingi vya utalii wakiwamo wanyama wa kila aina. Kuna tembo, chui, swala, twiga, simba, nyati, viboko ndege wa aina tofauti, nyoka na mijusi.

Mbali ya wanyama na ndege, kuna milima na mabonde, mito na maziwa bila kusahau ufukwe mrefu wa Bahari ya Hindi. Pamoja navyo, kuna maua, wadudu na miti ya aina tofauti.

Pamoja na wingi wa vivutio vilivyopo, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazonufaika kidogo kutokana na sekta ya utalii na moja ya sababu za hali hiyo ni idadi ndogo ya watalii wanaotembelea vivutio vingi vilivyopo.

Kuna sababu nyingi, nyingine za sekta hii kutokuwa na mchango unaotarajiwa ikiwamo ya ushiriki mdogo wa Watanzania kutembelea vivutio vyao licha ya mipango na mikakati lukuki iliyopo kuwahamasisha. Ukichunguza kwa umakini utabaini wananchi wengi wanapenda kuvifahamu vivutio tulivyopo nchini kama kuwaona wanyama, kupanda milima mirefu zaidi na hata kuogelea kwenye mito, maziwa au bahari lakini wanakosa fursa za kufanya hivyo.

Hili linajidhihirisha kwenye maonyesho haya ya Sabasaba ambako wananchi walionekana wakigombea kupiga picha na simba, lakini hawaonekani kwenye mbuga za wanyama zilizopo katika maeneo tofauti.

Ukitathmini sababu za watu kugombea kuwaona wanyama walioletwa kwenye Viwanja vya Julius Nyerere yanakofanyika maonyesho hayo, utagundua uwezo, utayari na hamasa waliyonayo kuvifahamu na kuviona vivutio vyao.

Kwa baadhi ya washiriki, uzuri wa maonyesho hayo ni kuona wanyama walioletwa kutoka mbugani wanakohifadhiwa. Wapo waliotoka jijini Dar es Salaam licha ya maeneo wanakotoka kuwa jirani, lakini watu hawaendi kuwaona wakiwa katika maeneo ya asili zao.

Msongamano wa kuwashuhudia wanyama hao na baadhi ya watu kusukumana ili waingie mahali walipo ni jambo la linalotafakarisha. Washiriki walionekana wakiwa katika foleni na hawakulalamika na wakati mwingine mashine za kukatia tiketi zilielemewa na kuwalazimu maofisa waliopo kuongeza nyingine.

Pupa hii ya kutaka kuingia katika banda hilo isichukuliwe kama ni jambo la kawaida tu. Tunaamini kwamba mamlaka husika kuanzia wizara na taasisi zilizo chini yake zitaiona fursa hii ya kukuza utalii wa ndani na kuangalia sababu zilizowavutia watu kwenda kuwaona na kupiga picha na simba wa Sabasaba, lakini hawafanyi hivyo kwenye mbuga wanakoishi na kuifanyia kazi.

Lililo wazi ni kwamba Watanzania wanapenda kutalii, isipokuwa kuna vikwazo vingi vinawakwamisha. Kama mtu anatoka Bagamoyo hadi Viwanja vya Mwalimu Nyerere, kwa nini anashindwa kwenda Hifadhi ya Saadan iliyopo wilayani humo?