Kwamba mtu mmoja amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa kipindupindu jijini Dar es Salaam huku wengine 32 wakilazwa katika kambi maalumu kwa maradhi hayo ni habari za kusikitisha.

Mbali na kipindupindu, ugonjwa mwingine wa homa ya dengue nao unaendelea kuwatesa maelefu ya Watanzania katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Singida huku takwimu zilizopo zikionyesha kwamba watu wawili wamepoteza maisha.

Tunasikitishwa na taarifa za kusambaa kwa maradhi haya yanayogharimu maisha ya watu na maumivu makali kwa kuwa tunaweza kabisa kupambana nayo na kuyatokomeza kabisa, kukiwa na mipango, dhamira na ushirikiano wa wadau wote.

Jana, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwa katika ziara jijini Dar es Salaam kuangalia hali ya ugonjwa wa kipindupindu na homa ya dengue alikaririwa akisema kati ya wagonjwa hao 32, kambi ya Amana wapo 13, Temeke 18 na Mwananyamala mmoja na kwamba hali hiyo imetokana na kutozingatia usafi.

Kwa sababu hiyo, alizitaka halmashauri zote za Mkoa wa Dar es Salaam kutoa adhabu kali kwa watu wanaotiririsha maji machafu hasa wakati wa mvua. Akisema adhabu iliyopo ya Sh30,000 ni ndogo na angependa iwe Sh200,000 ili wahusika waone ni bora kuita gari la majitaka kwa Sh150,000.

Tunafahamu kwamba kauli ya waziri inatokana na kukerwa kwake na uzembe na tabia ya kutiririsha majitaka wakati mvua kubwa zinaponyesha kitendo ambacho kina mchango mkubwa katika kueneza kipindupindu.

Ugonjwa wa kipindupindu unatokana na kinyesi na ndiyo sababu waziri Ummy amekerwa na tabia ya watu wanaotiririsha majitaka.

Kwa mujibu wa wataalamu, homa ya dengue inaambukizwa na virusi vya mbu aina ya Aedes ambao ni weusi wenye madoadoa meupe yenye kung’aa. Mbu hao hupendelea kutaga mayai kwenye maji yaliyotuama hasa kwenye makopo ya maua. Pia, hupendelea makopo yenye rangi nzito yaliyo kwenye eneo lenye giza au makasha yaliyo wazi.

Kwa ujumla, sababu zinazoeneza maradhi haya zinatokana na uchafu wa mazingira kwa maana hiyo zipo mikononi mwetu kama familia, uongozi wa mtaa/kijiji, kata, tarafa, wilaya na hata mkoa na taifa kwa ujumla.

Tunasema hivyo tukimaanisha kwamba ikiwa familia au wakazi katika kila nyumba watachukua hatua na kusafisha maeneo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba hakuna maji yanayotuama katika maeneo mbalimbali kama ilivyobainishwa na pia kuacha tabia ya kutiririsha majitaka, tutayashinda maradhi haya kirahisi kabisa.

Lakini wakionekana kutochukua hatua ilhali maeneo yao ni machafu, viongozi kuanzia ngazi za mtaa kwenda juu wanapaswa kuchukua hatua kuhakikisha kwamba maeneo husika yanakuwa safi.

Mathalan, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Yudas Ndungile jana alikaririwa akisema sehemu kubwa ya wagonjwa wa kipindupindu waliopatikana wanatoka katika eneo la Mchikichini na mabondeni ambako magari ya kusomba taka hayapo. Jambo la kujiuliza hapo ni kwamba familia hizo zimeelimishwa kwa kiasi gani kuhusu hatari ya maisha yao dhidi uchafu wa mazingira?

Je, ngazi nyingine za juu na wadau wamechukua hatua gani kuzuia majanga yatokanayo na uchafu huo hasa ikizingatiwa kwamba tiba yake ina gharama kubwa za hali na mali ikilinganishwa na kinga.