In Summary
  • Mjamzito huyo, Amina Mbunda anasema awali mgambo walifika kwake na kumueleza mumewe amenunua kitanda cha wizi, lakini alipowaeleza kwamba hayupo waliondoka. Mbunda anasema saa chache baada ya mgambo hao kuondoka, mwenyekiti wa kitongoji, mwanamume mmoja na polisi walifika nyumbani kwake na kumkamata wakidai watamuachia hadi mtuhumiwa atakapopatikana.

Kitendo kilichofanywa na askari wa Kituo cha Polisi cha Mang’ula mkoani Morogoro cha kumuweka mahabusu mwanamke mjamzito kwa takriban saa kumi hakikubaliki. Mjamzito huyo mkazi wa Mang’ula alikamatwa na polisi kwa madai kuwa mumewe amenunua kitanda cha wizi.

Mjamzito huyo, Amina Mbunda anasema awali mgambo walifika kwake na kumueleza mumewe amenunua kitanda cha wizi, lakini alipowaeleza kwamba hayupo waliondoka. Mbunda anasema saa chache baada ya mgambo hao kuondoka, mwenyekiti wa kitongoji, mwanamume mmoja na polisi walifika nyumbani kwake na kumkamata wakidai watamuachia hadi mtuhumiwa atakapopatikana.

Kinachosikitisha ni kitendo cha polisi hao kumuweka mahabusu kwa saa kumi mjamzito huyo ambaye baadaye alizidiwa kwa kushikwa uchungu. Tunaamini polisi hao hawakuwa na sababu ya msingi kumuweka ndani kwa kuwa moja ya majukumu yao ni kulinda usalama wa raia na kuwasaidia wanapokuwa na matatizo.

Mbunda hakuwa mtuhumiwa wa kununua kitanda cha wizi, kwa mantiki hiyo amewekwa mahabusu kwa kosa ambalo halimhusu. Lakini, kinachoshangaza polisi hao huwa wanatoa fursa kwa baadhi ya watuhumiwa kujidhamini, walishindwaje kutumia busara na kumruhusu mjamzito huyo ajidhamini kama waliamini ana makosa?

Tukio hilo ni mwendelezo wa askari polisi kushindwa kutumia busara, hivi karibuni wakati wa tetesi za maandamano ya Aprili 26, jijini Dar es Salaam mama aliyekuwa akimuuguza mtoto wake hospitali alikamatwa na polisi na kuswekwa mahabusu na mwanawe aliyekuwa mgonjwa.

Pia, mkoani Mwanza mama mwenye mtoto wa umri wa miezi sita aliwekwa mahabusu na mwanaye ambaye alifariki dunia baadaye na kuzua taharuki kwa jamii katika eneo la Nyegezi mkoani humo.

Thamani ya Jeshi la Polisi ni uadilifu na kutoa haki kwa raia, lakini kubwa zaidi ni kutumia busara na hii inakumbusha kesi ya Novemba 2002 ya askari polisi wa Kituo cha Rujewa wilayani Mbarali mkoani Mbeya, waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya mahabusu 17 kati ya 112 waliokuwa wamesongamana kwenye chumba kidogo na kukosa hewa.

Mahakama ilishangazwa na askari waliokuwa zamu kushindwa kutumia busara kuokoa maisha ya mahabusu hao kwa kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kila mtu ana haki ya kuishi.

Pamoja na taarifa kwamba Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa tukio la Mang’ula, bado kuna haja ya kulaani kitendo hicho ambacho si cha kibinadamu na hakiendani na utendaji kazi wa weledi ndani ya jeshi hilo. Tunasema hivyo kutokana na mlolongo wa matukio yasio kuwa na busara yanayofanywa na askari polisi.

Lakini, wananchi nao ni muhimu wakazitambua haki zao mbele ya polisi ikiwamo haki ya kujulishwa sababu za kutiliwa shaka au kukamatwa.

Tunachojiuliza polisi aliyekwenda kumkamata Mbunda alimpa haki ya kuwajulisha ndugu na jamaa kwamba amekamatwa na polisi. Kwa maana kama hilo lingefanyika mjamzito huyo angeweza kunusurika na kadhia iliyomkuta ya kujifungulia sehemu isiyostahiki.

Rai yetu kwa Jeshi la Polisi na hasa askari wake wajitathmini katika utendaji wao wa kazi, kitendo kilichotokea Mang’ula kingeweza kuzuilika kama polisi wangemsaidia mjamzito huyo kwa kumuwahisha hospitali au kujua mapema historia ya ujauzito wake. Wakati tunaotoa rai hiyo pia askari aliyehusika kumkamata mjamzito huyo anapaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu, kwa kuwa kitendo chake kimechafua sifa ya jeshi hilo.