Februari Mosi, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima aliamuru kuwekwa mahabusu Diwani wa Susuni (Chadema), Abiud Solomon kwa madai ya kuonyesha dharau kwenye kikao chake cha kumtambulisha mkuu mpya wa Wilaya ya Tarime, Charles Kabeho.

Hata hivyo, diwani huyo alisema dharau anayodaiwa kuifanya ni kubebanisha miguu yake (kuweka nne), lakini Malima anasema diwani alimdharau kwa kukaa huku akiwa ameegemea kiti na miguu yake akiwa ameiweka juu ya meza.

Malima alitoa amri hiyo ikiwa ni siku mbili baada ya Rais John Magufuli kubainisha kwamba kuna baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa wanatumia vibaya nafasi zao za uongozi kwa kuwaweka watu mahabusu hata pale makosa wanayotuhumiwa nayo ni ya kawaida.

Mbali na Rais Magufuli, wengine waliowahi kuwaonya wateule hao ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Pia, mawaziri Selemani Jafo (Tamisemi), George Mkuchika (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) na Ummy Mwalimu (Afya) wamewahi kuonya.

Mbali ya kuwaonya, lakini Rais Magufuli alihoji inakuwaje mtu awekwe mahabusu kwa kutumia Sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ya 1997, lakini kesho yake asifikishwe mahakamani?

Pia, alisema anajua wakuu hao wa mikoa na wilaya wameshaonywa mara kadhaa, lakini hawajaacha huku akibainisha kuwa kuna masuala mengi hayahitaji kuwaweka watu mahabusu, bali yanahitaji kutoa maelekezo.

Tunaendelea kuiona kauli ya Rais Magufuli kuwa ni agizo linalopaswa kuzingatiwa na viongozi hao kwa kuacha papara katika kutoa uamuzi hasa inayoleta maumivu kwa upande unaotuhumiwa.

Kwa mfano, sababu iliyotolewa na diwani Solomon na ile iliyotolewa na Malima ni kama alivyosema Rais Magufuli kwamba, masuala mengine yanahitaji kutoa maelekezo tu na si vinginevyo.

Kinachoshangaza ni kuwa, baadhi ya wateule hao wamekuwa wepesi kuwaweka watu mahabusu, lakini kuna masuala ya msingi yanayohusu matatizo ya wananchi ambayo hatuwaoni wakiyatolea kauli nzito.

Mfano wa hivi karibuni ni katika Wilaya ya Mafinga mkoani Iringa ambako kinamama walilalamikia mtuhumiwa wa ubakaji kutokamatwa, jambo lililomlazimu Rais kuingilia kati ilhali viongozi wa wilaya wapo na hakuna hatua waliyochukua.

Tunaamini kwamba viongozi wa mikoa na wilaya wamekwishamsikia kiongozi huyo mkuu wa nchi ambaye siku zote amekuwa akisisitiza utoaji wa haki na kutetea wanyonge. Hatuamini kwamba kuna mkuu wa mkoa au wa wilaya ambaye hakuielewa kauli yake Januari 29, kuhusu sheria ya kuweka watu ndani aliyoitoa baada ya kuwaapisha majaji 15 wa Mahakama Kuu na sita wa Mahakama ya Rufani.

Pia, tunaamini kwa kuwa tukio la kuwaapisha majaji hao ikiwamo hotuba ya Rais Magufuli ilionyeshwa mubashara na baadhi ya vyombo vya habari, wateule wengi wa mkuu wa nchi waliupata ujumbe wake.

Viongozi wote wa umma wanafahamu kauli inayotolewa na mkuu wa nchi ni maelekezo kwao, hivyo hatuamini kama kuna mteule yeyote anayeweza kwenda kinyume na aliyemteua.

Rai yetu kwa viongozi wafuate maelekeo wanayopewa na wakubwa zao, kwani kuonyesha ubabe kwenye utendaji ni kwenda kinyume na maadili ambayo waliapa kuyalinda.