In Summary
  • Manji amekuwa kiongozi mwenye mafanikio Yanga kwa kuiwezesha timu hiyo kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara mfululizo

Uamuzi wa mfanyabiashara Yusuph Manji kurejea kwenye nafasi ya uenyekiti Yanga unatajwa kama suluhisho la muda mfupi la kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili klabu hiyo katika siku za hivi karibuni.

Tangu Manji alipotangaza kujiweka kando katika nafasi hiyo mwezi Mei mwaka huu, Yanga imekuwa ikipita katika milima na mabonde ambayo idadi kubwa ya wadau wa soka wamekuwa wakiihusisha moja kwa moja na kukosekana kwake klabuni.

Kabla ya kuanza kwa msimu huu, Yanga ilijikuta ikiwa na deni linalotajwa kuwa zaidi ya Sh200 milioni, ambalo lilitokana na madai ya posho na mishahara ya wachezaji na benchi la ufundi katika kikosi chake ambacho kilitetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo katika msimu uliopita wa 2016/2017.

Yanga iliwapoteza Vincent Bossou, Deus Kaseke na Haruna Niyonzima ambao walitimka baada ya kushindwa kuafikiana dau la kuongeza kusaini mikataba mipya baada ya ile ya awali kumalizika, lakini pia iliwakosa baadhi ya nyota wapya iliyotegemea kuwasajili kutokana na kuzidiwa kete na baadhi ya timu pinzani.

Mbali na hilo, Yanga ililazimika kutofanya usajili mkubwa huku ikitumia fedha kiduchu katika dirisha kubwa la usajili tofauti na ilivyokuwa ikifanya miaka ya nyuma.

Jinamizi hilo limeonekana kuendelea kuisumbua Yanga katika ligi, pamoja na kutofungwa mechi yoyote hadi sasa, bado imekuwa haionyeshi kiwango bora uwanjani, jambo linalohusishwa na kupungua morali kwa wachezaji wake kutokana na hali ngumu ya kifedha waliyonayo.

Kuthibitisha namna gani Yanga kwa sasa nguvu yake ya kiuchumi imepungua, hivi karibuni ilianzisha utaratibu wa kuwashirikisha wanachama wake katika kuchangia gharama za ukarabati wa Uwanja wa Kaunda ili utumike kwa mazoezi ya timu hiyo huku kukiwepo na mpango wa ukarabati wa hosteli zake zilizopo katika makao makuu eneo la Jangwani.

Hata hivyo, wadau mbalimbali wa soka wameliambia gazeti hili kuwa hakuna mtu anayeweza kumaliza matatizo na changamoto zote zinazoikabili Yanga zaidi ya Manji, hivyo ni jambo la busara kwake kurejea klabuni ili airudishe kwenye mstari.

“Kiukweli mwenyekiti ni mtu muhimu kwa klabu hii kwa sababu katika kipindi chake chote ameijitolea fedha na muda mwingi kuhakikisha mambo yanakwenda sawa na hakuna namna unayoweza kutaja mafanikio ya Yanga bila kumhusisha mwenyekiti, Manji.

“Ndio maana unaona wajumbe wa kamati ya utendaji pamoja na wanachama tumekuwa ukiendelea kumuomba arejee na hata barua yake ya kujiuzulu, viongozi wa matawi hawakukubaliana nayo kwa lengo la kumsihi abakie kwenye nafasi yake.

“Hivyo bado anahitajika na kila Mwanayanga anayeitakia mema klabu anapenda kuona akirejea,” alisema kaimu mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga.

Mwanachama wa Yanga, Kais Edwin Mwasongwe mwenye kadi namba 005900 alisema kurejea kwa Manji ndani ya klabu hiyo ni suala lisilohitaji mjadala na hawatokubali kuona akiwa nje ya timu hiyo.

“Kikubwa cha kwanza ambacho ninaweza kukisema ni kuwa mimi na wanachama wote halali wa Yanga tunatambua bado Manji ni mwenyekiti wa klabu yetu na sio vinginevyo.

“Hapo katika kipindi cha katikati amepitia katika nyakati ngumu ambazo binadamu yeyote angehitaji kupumzika. Kwa sababu alifanya vile ili kulinda hadhi yake na heshima ya Yanga kutokana na tuhuma zilizoelekezwa kwake.

“Lakini pili baada ya ndugu Yusuph Manji kutangaza kujiuzulu, sisi viongozi wa matawi tulipinga barua yake na tulimpa nafasi tu ya kumpumzika jambo ambalo tunashukuru hata kamati ya utendaji ilituunga mkono kwa sababu katiba ya Yanga ina kipengele ambacho kinawapa haki wanachama kupinga kujiuzulu kwake.

“Kikubwa kinachofuata sasa kwa mujibu wa katiba yetu ni kuitisha mkutano wa wanachama, ambao watajadili barua yetu viongozi wa matawi na ile ya kamati ya utendaji kupinga kujiuzulu kwake pamoja na barua yake mwenyekiti na ikibidi kumualika kwenye mkutano ili apate fursa ya kutoa maoni yake.

“Kama wanachama wakiridhia ajiuzulu au asijiuzulu, ni mkutano mkuu ndio utaamua lakini kwa hali halisi ni kuwa hakuna asiyemhitaji Manji ndani ya klabu yetu lakini pia hata mazingira tunayokabiliana nayo kwa sasa ni Manji ndiye anaweza kutuondoa,” alisema Kais, ambaye ni mmoja wa viongozi wa matawi.