In Summary
  • Yanga ni bingwa mara 26 wa Ligi Kuu Bara msimu huu imeanza ligi vibaya

Kocha  Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema kuwa wale wanaoibeza timu yake kutokana na matokeo waliyoyapata katika mechi zilizopita, wasubiri kuona wakifufukia kwa Yanga.

Kagera haijaonja ushindi wowote katika mechi zake tano za Ligi Kuu na kesho, Jumamosi watakuwa nyumbani kuwakaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao sita msimu uliopita.

Maxime alisema wapo baadhi ya wadau wa soka wanaoibeza timu hiyo kutokana na matokeo mabovu iliyopata na kwamba, wamejiandaa kuhakikisha wanafufukia kwa Yanga kwa ushindi ili kurejesha matumaini kwa mashabiki wake.

Alisema kuwa maandalizi waliyoyafanya wameridhikana nayo na kusema kwamba vijana wote wana ari nzuri, isipokuwa wale ambao ni majeruhi wa muda mrefu akiwamo George Kavila na Mohamed Fakhi ambao hawatacheza.

“Ni kweli matokeo yetu hayaridhishi, lakini niwaambie hivi Kagera Sugar itafufukia kwa Yanga, najua wamekuja wakiamini kwamba hatuko vizuri, ila watakipata Jumamosi,” alisema Maxime.

Kocha huyo bora wa msimu uliopita, alisema kuwa licha ya kupata matokeo yasiyoridhisha, lakini kiufundi timu inacheza vizuri na kwamba mabao wanayofungwa ni kama ya miujiza tu.

Aliongeza kuwa haoni timu yoyote kwenye ligi kuu yenye wachezaji wazuri kama Kagera Sugar, hivyo kutokana na hali hiyo anaamini wakianza kushinda hawapotezi tena.

“Kwanza miongoni mwa timu za ligi kuu,sioni hata moja yenye kiwango kama Kagera Sugar, haya matokeo ni mapito tu na siku tukianza kushinda ndio watu watatujua,” alitamba Kocha huyo.

Katika msimamo wa ligi kuu, Kagera Sugar ipo mkiani kwa pointi mbili, huku Yanga wakiwa nafasi ya sita kwa alama tisa baada ya kucheza mechi tano kila timu.