In Summary
  • Uwanja wa Kaunda ulijengwa mwaka 1973 kwa gharama ya Sh 3milioni  ambazo zilipatikana kwa michango kutoka kwa taasisi mbalimbali na wahisani wengine.

Dar es Salaam. Uongozi wa Yanga umeendelea kujaza vifusi kwenye uwanja wao wa Kaunda katika jitihada za kutimiza ndoto kurudisha hadhi ya kiwanja hicho.

Ofisa habari wa Yanga, Dismas Ten alisema uwanja huo unahitaji kumwagwa vifusi 2250, ili kuenea katika eneo lote la uwanja na maalekezo hayo wamepewa na kamati ya ujenzi iliyokuwa chini ya Kaimu Mwenyekiti Clement Sanga.

Ten alisema kuna mipango mingi ambayo wameiweka katika uongozi huo, lakini kwa sasa kuna mambo makubwa mawili yanaendelea la kujenga uwanja mdogo wa kisasa na kurekebisha jengo la klabu kuwa la kisasa na kutumika katika matumiza ya klabu kama ilivyokuwa zamani.

“Mpaka sasa tumeshamwaga robo ya vifusi katika ile idadi ambayo tulikuwa tunaitaka, lakini tunaomba wapenzi na hata ambao si wapenzi wa Yanga kujitokeza katika zoezi la kumwaga vifusi katika eneo hilo kwani hilo jambo ni la kimaendeleo ya soka hapa nchini,” alisema.

“Gharama za matangenezo ya uwanja mpaka unakamilika hatutakuwa nayo kwani kwa sasa tupo katika hatua ya kwanza ya kumwaga vifusi ambavyo kuna watu wanatupatia bure, lakini wengine tunawapoza,” alisema.

“Tukija katika hatua ya pili ambayo itakuwa kabla ya dirisha dogo la usajili hatua ya kuotesha nyasi kamati ya ujenzi itakuwa na waandisi ambao wanaweza kutoa takwimu sahihi ya pesa ambayo imetumika au itatumika mpaka mwisho wa ujenzi wa uwanja na marekebisho ya jengo la klabu,” alisema Ten.