Dar es Salaam. Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga inatarajia kuweka kambi kisiwani Pemba kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba utakaochezwa Agosti 23 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Taarifa kutoka ndani ya  Yanga inasema klabu hiyo itacheza mechi ya kirafiki na Mlandege Jumapili kisiwani Unguja kabla ya kwenda Pemba.

"Mara baada ya mchezo dhidi ya Mlandege siku ya Jumapili, kikosi chetu kitaelekea Pemba kuweka kambi," imesema taarifa ya Yanga ikimnukuu Katibu Mkuu Charles Boniface Mkwasa.

Mchezo wa Simba na Yanga umeanza kuwa gumzo kwa mashabiki wa timu hizo kutokana na usajili mkubwa uliofanywa na watani hao wa jadi msimu huu.