In Summary
  • Ligi Ndogo ya wanawake ndiyo itakayotoa timu zitakazocheza Ligi Kuu

 Uongozi wa Timu ya Tanzanite ya Arusha inayoshiriki ligi ndogo ya wanawake katika kituo cha Dar es Salaam, umekata rufaa kupinga mtokeo ya Simba Queens waliyopata katika mchezo wa mwisho wa ligi hiyo.

Kocha Mkuu wa Tanzanite, Juma Masoud alisema  katika mchezo huo uliopigwa katika uwanja wa Karume na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 walihujumiwa na viongozi waliosimamia kituo hicho pamoja na waamuzi wa mchezo.

“Tangu awali tuliona dalili ya Simba kupewa ushindi kwani waamuzi wa mchezo huo walianza kujichanganya wao mapema kabla ya mchezo kwa kushiriki chakula cha pamoja na timu ya Simba” alisema Masoud.

Aliongeza kuwa kabla ya mchezo kuanza alifuatwa na viongozi waliosimamia kundi hilo wakimtahadhalisha baadhi ya wachezaji wake wasitumike katika mchezo huo kwa kuwa hawapo kihalali kwenye timu hiyo.

“Wakati tunarumbana, timu ndio zilikuwa zinaingia uwanjani, wao kama walijua wachezaji wangu mamruki kwanini wasiache mchezo umalizike ndipo kanuni zifuatwe na sio kuwazuia wachezaji wangu, hatukubali mchezo lazima urudiwe” alihoji Kocha huyo.

Hata hivyo alisema kuwa baada ya mchezo kumalizika walipata ushahidi ambao wameuwasilisha katika ngazi za juu kwa Simba kuwatumia wachezaji ambao si wa timu hiyo.

Pamoja na kutowataja wachezaji hao wa Simba wala wale wa Tanzanite, Timu hiyo ilikuwa inahitaji sare pekee ili kujihakikishia kucheza Ligi kuu, kwani katika michezo yake ya awali aliifunga timu ya Morogoro Sisters kwa bao 1-0 kisha kuisambaratisha Kisarawe Queens mabao 15-0 , huku Simba ikianza na Kisarawe kwa mabao 8-0, na kuilaza Morogoro Sisters mabao 5-3.

Hata hivyo Katibu Mkuu wa Chama cha soka la Wanawake Taifa (TWFA) Somoe Ng’itu alisema kuwa suala hilo bado halijafika katika ofisi yake ila litakapofika litafanyiwa kazi mara moja.

“Ninachokifahamu timu ya Simba ndio ilianza kuikatia Tanzanite rufaa na baadaye Tanzanite nao wakafuata, lakini ni ripoti ambayo inaenda kwa kamisaa wa mchezo na baadaye anaipeleka kwenye kamati ya mashindano kwa uamuzi zaidi."