In Summary

Klabu hiyo ipo katika harakati za kusaka kupanda kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao

Mwanza. Klabu ya Rhino Rangers imepanga kuwatupia virago wachezaji wake watatu na kusajili watatu likapofunguliwa dirisha dogo kesho.

Rhino Rangers ipo nafasi ya saba katika Kundi C ikiwa na pointi nane baada ya kucheza mechi tisa za Ligi Daraja la Kwanza mzunguko wa pili.

Kocha Msaidizi wa Rhino, Danny Mang’ombe alisema kwa tathmini waliyoifanya benchi la ufundi wamebaini kuwapo mapungufu kwenye eneo la ushambuliaji hivyo watahakikisha wanaongeza nyota watatu kutibu tatizo hilo.

Alisema kuwa watakaoongezwa ni wale wenye uzoefu, nidhamu na uwezo wa kucheza soka na kwamba wanatarajia kuangalia kwenye ligi Daraja la kwanza na ligi kuu.

“Kwa ujumla tumekuwa na tatizo kwenye umaliziaji, kwahiyo benchi la ufundi tutahakikisha tunaongeza wachezaji watatu wenye uwezo na uzoefu na tutaacha wengine watatu katika nafasi tofauti”alisema Mang’ombe.

Kocha huyo alibainisha kuwa matarajio yao yalikuwa kwenda mapumziko wakiwa nafasi tatu za juu, lakini ugumu wa ligi umesababisha kuwa nafasi mbaya hivyo wakirudi watafanya kweli.

“Malengo yetu ilikuwa ni kumaliza raundi hii tukiwa nafasi mbili au tatu za juu ila ligi imekuwa ngumu, bado hatujakata tamaa, tunaenda kujipanga ili tukirudi tufanye kweli,”alisema kocha huyo.