In Summary
  • Kiungo huyo amekuwa nje ya uwanja tangu alipoumia Septemba wakati akicheza mechi ya Europa Ligi

Manchester, England.KIUNGO wa Manchester United, Paul Pogba anakaribia kurudi uwanjani lakini viongozi wa klabu hiyo wameonywa kuwa kumchezesha dhidi ya Newcastle Jumamosi itakuwa ni haraka mno.

Pogba amekuwa nje ya uwanja kwa wiki nane ambapo amekosa jumla ya mechi 12 za Manchester United. Pogba aliumia misuli katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Basle, Septemba 12.

Mchezaji huyo raia wa Ufaransa alirudi katika uwanja wa mazoezi wa  Carrington mwishoni mwa mwezi uliopita baada ya kutumia muda mwingi akiwa Miami ambapo alikuwa akiuguza maumivu yake.

Wiki iliyopita alifanya mazoezi ya uhakika na kikosi cha pili na ikaonekana kwamba yupo fiti. 

Ingawa kocha wa Man United, Jose Mourinho ana shauku ya kumrudisha Pogba katika kikosi cha kwanza wadau wamemwambia kwamba itakuwa ni kucheza patapotea kwani anaweza kujitonesha.

Wanasema ni mapema sana kwa nyota huyo kuchezea kikosi cha kwanza kwani hajakuwa na utimamu wa mwili na kwamba  mechi sahihi ingetakiwa kuwa dhidi ya  Brighton, Novemba 25.

Manchester United kwa sasa ipo nyuma ya wapinzani wao Man City kwa pointi nane na kocha ana shauku kubwa ya kuona anachezesha kikosi chenye kasi kubwa ili awakimbize wapinzani wake.