In Summary
  • Timu za Arusha zimelazimika kuutumia Uwanja wa Ushirika Moshi kwa ajili ya mechi za Ligi Daraja la Kwanza na Pili baada ya wamiliki wa Sheikh

Arusha: Uongozi wa Timu ya Pepsi FC ya mjini hapa inayoshiriki Ligi Daraja la Pili (SDL) nao wamepeleka ombi lao kwa uongozi wa Uwanja wa Ushirika Mjini Moshi ili waweze kuutumia uwanja huo kwa michezo yao ya nyumbani kwenye ligi hiyo.

Meneja wa timu hiyo, Enock Nyongole alisema kuwa baada ya harakati zao kugonga mwamba walizokuwa wanataka kuzifanya ili kuhamia Morogoro katika Uwanja wa Jamhuri au Pwani katika Uwanja wa Mabatini.

“Baada ya uongozi kukaa tukaona hakuna sababu ya kuhamia mikoa hiyo kwani, timu zote tunazopambana nazo zipo ukanda wa Kaskazini isipokuwa Africans Sports ya Tanga, hivyo kwenda kwetu Morogoro au Pwani tungejiongezea gharama zisizo na maana,” alisema Nyongole.

Pepsi yenye Pointi mbili katika SDL baada ya kutoa sare ya bao 1-1 na Madini kisha na AFC Arusha itasafiri kuelekea mkoani Tanga mwishoni mwa wiki kukipiga na Africans Sports yenye pointi moja katika dimba la Mkwakwani.

Baada ya kufungwa kwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid timu hiyo inayonolewa na Kocha Richard Mbuya ilikuwa inasaka uwanja wake wa nyumbani jukumu ambalo kocha aliwaachia viongozi wa juu wa timu hiyo.

Endapo timu ya Pepsi itakubaliwa kuutumia Uwanja wa Ushrika, itakamilisha idadi ya timu saba zinazoutumia uwanja huo na hata ratiba za Ligi ya FDL na SDL Kuweza kubadilika kila mara hasa kundi B la SDL kutokana na ufinyu wa viwanja vinavyokithi Mahitaji.

Timu nyingine zinazotumia Uwanja wa Ushirika ni JKT Oljoro na Polisi Tanzania zote za FDL, AFC Arusha na Kitayosce, na Kilimanjaro Heroes za Kilimanjaro zote za SDL, hivyo kuzifanya timu za mkoa huo kuona kila mchezo wapo nyumbani.