In Summary

Majeruhi yamemweka nje kwa miezi mwili na sasa ameanza kujifua

Mwanza. Mshambuliaji wa Mwadui FC, Salim Khamis amesema kwa sasa yupo fiti kuanza kukipiga baada ya kupona majeraha ya mguu aliyokuwa akisumbuliwa kwa takribani miezi mitatu.

Mshambuliaji huyo amecheza mechi moja ya ufunguzi dhidi ya Singida United na kufunga bao moja, kwa sasa ameanza mazoezi na wenzake.

Alisema amepoteza mechi nyingi na kuzidiwa na wapinzani wake kwenye mbio za kuwania kiatu cha mfungaji bora, atapambana kuhakikisha anaonyesha ushindani.

Hadi sasa, Emmanuel Okwi (Simba) anaongoza kwa mabao nane, Mohamed Rashid (Prison) mabao matano, Ibrahim Ajib (Yanga) manne sawa na Shiza Kichuya wa Simba.

 “Japo nimeachwa mechi nyingi, lakini lolote linaweza kutokea, bado sijakata tamaa naweza kuanza kucheza na nikafunga mabao kutokana na mchezo utakavyokuwa,”alisema Khamis.

Mshambuliaji huyo alisema anachosubiri ni maelekezo ya kocha kama ataweza kumpanga katika mechi ya Jumamosi dhidi ya Stand United.