In Summary
  • Mhispania huyo ni mmoja ya wachezaji bora wa tenisi kwa wanaume duniani

London, England. Mchezaji tenisi nguli duniani Rafael Nadal, ametupwa katika mashindano ya Nitto ATP.

Nadal alipoteza mchezo huo baada ya kufungwa seti 7-6, 6-7, 6-4 alipovaana na David Goffin juzi usiku kwenye Uwanja wa London 2 Arena, England.

Nguli huyo anayeshika nafasi ya kwanza kwa ubora duniani, alicheza mchezo huo katika mazigira magumu baada ya kupata maumivu ya goti.

Baada ya kumalizika mchezo huo, mchezaji huyo alisema alicheza katika mazingira magumu na hakufurahi kutokana na maumivu.

Mchezaji nyota mwingine Roger Federer anapewa nafasi ya kutwaa ubingwa, baada ya mpinzani wake mkubwa Nadal kushindwa katika fainali hizo.

Nadal raia wa Hispania alisema alishafikia uamuzi wa kujitoa katika michuano hiyo hata kama angeshinda kwa kuwa hakuwa fiti.

“Nilishaamua ningeshindwa au ningeshinda nisingeendelea na michuano hii kwasababu sifurahii,” alisema Nadal aliyecheza akiwa na maumivu kwa saa mbili na dakika 32 kabla ya Mbelgiji anayeshika nafasi ya saba kwa ubora duniani kupata ushindi.

Alisema hakutaka kuharibu rekodi nzuri aliyoweka msimu huu kwa kutumia siku mbili kufikiria michuano hiyo akiwa katika mazingira magumu ya maumivu.

Nafasi ya Nadal ambaye alisema na uhakika wachezaji waliobaki katika kundi lao wana kiwango bora akiwemo Pablo Busta anayetarajiwa kurithi mikoba yake.