In Summary
  • Uongozi wasema kwamba mara nyingi walipokuwa wanawasiliana na mwanariadha huyo juu ya kujumuika na wenzake kambini alikuwa anawajibu kwa ufupi kuwa atakuja muda wowote.

Arusha. Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthon Mtaka ameeleza kuwa mwanariadha Agustino Sulle aliyeondolewa kwenye kambi ya Taifa inayojiandaa na Mashindano ya Jumuiya ya Madola atakabiliwa na kifungo kama fundisho.

Alisema kuwa kama TOC na BMT wamejiridhisha kutokana na ripoti ya kocha na RT hawataweza kufumbia macho jambo hilo kwa kuwa watakuwa wanafuga uovu kwenye Shirikisho hilo.

Mtaka alisema kuwa wameingia ghalama kubwa kwa ajili ya kambi na watakapokaa ndipo wataamua adhabu gani itamkumba ikiwemo kutopewa kibali cha kwenda kwenye mashindano sambamba na kifungo kwa muda watakaoamua.

“Muda wote hakuwa kambini na amekuwa na taarifa ambazo za uongo na hata alipokuwa ameitwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) pamoja na RT bado alikuwa haeleweki kutokana na majibu yake,” alisema Mtaka.

 

Aliongeza kuwa msingi wake ni kutokana na mialiko yake binafsi alihofia akiwa kambini ataweza kuzuiliwa na alipogundua hilo akawa amechelewa kwa kuwa taarifa zilikuwa zimefika mbali na kushindwa hata kuomba ruhusa kwaajili ya mashindano yake.

“Shirikisho linawaacha huru wanariadha kushiriki mashindano yao na tunawapa sapoti lakini linapokuja suala la Taifa kila mmoja anatakiwa kushiriki ipasavyo.”

Hata hivyo kocha mkuu wa timu ya hiyo Zakaria Barie alisema kuwa kilichomponza mwanariadha Agustino Sulle kuenguliwa kikosini ni kutokana na kibuli chake.

 “Tulipoona siku zinazidi kusonga na haonekani tukabidi kumuuliza kocha wake Thomas Tlanka ambaye naye alitujibu tuwasiliane na mwanariadha mwenyewe kwani yeye hajui lolote juu ya kutoripoti kwake kambini” alisema Barie.

Aliongeza kuwa baada ya kuona hali hiyo inazidi ndipo walipoamua kutoa taarifa kwa viongozi wa juu ambao nao wameamua kumwondoa kabisa kambini kutokana na utovu wa nidhamu na itakuwa fundisho kwa wafukuza upepo wengine.