In Summary

Mwanariadha huyo wa mbio za 5,000 Mita amejumuishwa kwenye timu ya taifa ya riadha itakayopiga kambi Lushoto kujiandaa na michuano ya Jumuiya ya Madola yatakayofanyika Aprili mwakani nchini Australia.

Arusha. Mwanariadha Gabriel Geay ambaye alishindwa kushiriki mashindano ya Dunia yaliyofanyika London mwaka huu, huku Tanzania ikiondoka na medali ya shaba iliyoletwa na Alphonce Simbu katika mashindano ya Marathon, tayari ameanza kujifua.

Geay alishinda hata kuanza mbio hizo kutokana na maumivu ya goti lililokuwa likimsumbua tangu akiwa kambini Arusha lakini alikwenda kibishi London ili kuitetea Taifa lake kwenye michuano hiyo, kabla ya kunyanyua mikono juu sambamba na Magdalena Shauri aliyeishia njiani kwenye mbio ndefu.

“Nilipofika London kabla ya mashindano tulifanyiwa vipimo wanariadha wote ndipo daktari akanishauri nisisumbuke kushiriki mashindano yale kwa kuwa tatizo langu lilikuwa kubwa na endapo ningeshiriki historia yangu ya riadha ndio ilikuwa inaishia hapo,” alisema Geay.

Mara baada ya kurudi Nchini mwanariadha huyo aliendelea kuufuta ushauri wa Daktari wa kutofanya mazoezi yoyote ili apate muda mzuri wa kuupumzisha mwili wake kwa miezi kadhaa kabla ya kuanza mazoezi mepesi.

“Kwa muda wote nilikuwa nyumbani na mara chache nilikuwa nakwenda kumwona daktari kujua maendeleo ya mguu wangu na sasa namshukuru Mungu naendelea vizuri na tayari nimeanza mazoezi mepesi”

Hata hivyo ameeleza kuwa kwa sasa hataweza kujumuika na wenzake kambini hadi pale afya yake itakapotengemaa kisha atajumuika na wenzake tayari kwenda kuiwakilisha taifa kwenye mashindano ya Madola ambayo amepania kwenda kufanya vyema.