In Summary
  • Kocha huyo Mreno anataka kuimalisha safu ulinzi ili kutimiza ndoto yake ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England

London, England. Siku za beki Luke Shaw kubaki Manchester United zinahesabika, baada ya Jose Mourinho kurusha ndoano kwa kinda Enzo Diaz.

Licha ya umri mdogo, kocha huyo anataka kumsajili kuziba pengo la nafasi ya beki wa kushoto Man United.

Man United imeridhishwa na kiwango cha Diaz  anayecheza timu ya daraja la pili leaders Agropecuario nchini Argentina.

Mourinho amekosa beki wa uhakika wa kusghoto na amekuwa akiwatumia kwa nyakati tofauti Matteo Darmian, Ashley Young, Daley Blind na Shaw.

Baada ya kucheza mechi saba za ligi, kinda huyo mwenye uwezo pia wa kucheza nafasi ya beki wa kati, amekuwa kivutio kwa makocha akiwemo Mourimhi.

Shaw hana mpango wa kuondoka Man United licha ya kutakiwa na Fenerbahce akidai atapambana kupata namba kikosi cha kwanza Old Trafford.

Beki huyo alianza kupoteza namba baada ya kuvunjika mguu uliomuweka nje ya uwanja muda mrefu na aliporejea hakuwa chaguo la Mourinho.

Diaz alisema mwenye uamuzi wa kumtoa ni wakala wake na sasa anajikita katika klabu yake ingawa aliitaja Man United ambayo kila mchezaji ana ndoto ya kuitumikia.

“Wakala wangu ameniambia anataka kuniangalia katika mechi nyingi. Lakini ni ndoto ya kila mchezaji kucheza Manchester United,” alisema Diaz.

Msimu huu Shaw mwenye miaka 22, amecheza dakika 48 katika mchezo wenye ushindani, lakini mara zote amekuwa akiingia akitokea benchi. Beki huyo alitua Man United kwa Pauni 27 milioni mwaka 2014.