In Summary
  • Msimu uliopita Mbao ilifanikiwa kucheza fainali ya Kombe la FA

Mwanza. Safu ya ulinzi ya Mbao FC imeimarika baada ya kurejea kwa mabeki wake,Yusuph Mgeta na Yusuph Ndikumana kabla ya mchezo wake wa kesho Ijumaa dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Meneja wa Mbao FC, Faraji Muya alisema mchezo uliopita mabeki hao hawakucheza kutokana na sababu mbalimbali.

 “Mgeta alikuwa akisumbuliwa na homa na Ndikumana alikuwa akitumikia adhabu yake ya kadi tatu za njano na sasa wote watakuwa kuwepo uwanjani.

 “Kwa ujumla tupo fiti na kila mchezaji ana ari nzuri na kubwa zaidi wachezaji waliokosa mchezo uliopita kwa sababu mbalimbali wamerejea akiwamo Mgeta na Ndikumana,”alisema Muya.

Meneja huyo aliongeza hawatokuwa tayari kuruhusu tena sare au kupoteza na badala yake watapambana hadi kupata pointi tatu.

“Maandalizi wameyafanya ya kutosha hivyo wanaingia uwanjani kwa kuamini kwamba lazima washinde ili kujiweka nafasi nzuri kwenye msimamo.”