In Summary
  • Mbao FC ilitoka katika michezo ya sare ikiwa haina nyota hao waliokuwa majeruhi

 Kurejea kwa nyota wa Mbao FC, Yusuph Mgeta na Yusuph Ndikumana kumeipa kiburi timu hiyo kutamba kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa leo dhidi ya Mbeya City.

Mbao FC inatarajia kushuka Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, huku ikiwa na kumbukumbu ya kufululiza sare dhidi ya Simba na Prisons kwenye mfululizo wa mechi zake za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Meneja wa Mbao FC, Faraji Muya alisema mchezo uliopita mabeki hao hawakucheza kutokana na sababu mbalimbali na Mgeta alikuwa akisumbuliwa na homa.

Muya alisema kwa upande wa Ndikumana alikuwa akitumikia adhabu yake ya kadi tatu za njano na sasa mchezo wa leo utawarejesha nyota hao wote wakisaka ushindi.

“Kwa ujumla tupo fiti na kila mchezaji ana ariya juu na zaidi wachezaji waliokosa mchezo uliopita kwa sababu mbalimbali wamerejea akiwamo Mgeta na Ndikumana,” alisema Muya.

Meneja huyo aliongeza kuwa licha ya mchezo huo kuwa na ushindani, lakini hawatokuwa tayari kuruhusu tena sare au kupoteza na badala yake watapambana hadi wanabaki na pointi tatu.

Aliongeza kuwa kama ni maandalizi wameyafanya ya kutosha, hivyo wanaingia uwanjani kwa kuamini kwamba lazima washinde ili kujiweka nafasi nzuri kwenye msimamo.