In Summary
  • Wachezaji hao huenda wakaa nje kwa muda mrefu kutokana na kuumia

London, England. Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp ana hofu ya kuwakosa nyota wake Sadio Mane na Nathaniel Clyne muda mrefu.

Mane na Clyne wanaweza kuwa nje ya uwanja muda mrefu, baada ya kupata maumivu ambayo yanaweza kuigharimu Liverpool katika mashindano inayoikabili.

“Tutamchunguza Sadio kujua ukubwa wa jeraha lake na madaktari watatoa taarifa,” alisema kocha huyo wa zamani wa Borussia Dortmund ya Ujerumani.

Mane aliumia misuli katika mchezo wa timu ya taifa ambao Senegal iliichapa Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ na kukata tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia nchini Russia mwakani.

 

Clyne anatarajiwa kuwa ya uwanja zaidi ya miezi mitatu, baada ya kufanyiwa upasuaji ambao utamuweka nje ya uwanja muda mrefu.

Klopp alisema hilo ni pigo katika kampeni ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu kwa kuwa nyota hao ni tegemeo lake katika kikosi cha kwanza.

Mane amekuwa na mchango mkubwa katika kikosi hicho baada ya kufunga mabao 16 katika mechi 32 alizocheza tangu alipojiunga na klabu hiyo majira ya kianagzi msimu uliopita.

Liverpool ilishituka baada ya kiungo huyo wa pembeni kurejea haraka London muda mfupi baada ya mchezo wao na Afrika Kusini walioshinda mabao 2-0.

“Tatizo la nyama limekuwa ajenda kwa mara nyingine. Ni vigumu sana kuzuia hali hii,” alisema Klopp.