In Summary
  • Cameroon 'The Indomitable' ilichakazwa na mabingwa hao wa Amerika Kusini katika mchezo huo wa kwanza wa Kundi B wa mashindano hayo.

Kocha wa Cameroon, Hugo Broos amekisifu kikosi chake kwa kuonyesha soka ya kiwango cha juu dhidi ya Chile pamoja na kupokea kipigo cha mabao 2-0, katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Fifa yanayoendelea Moscow, Russia.

Cameroon 'The Indomitable' ilichakazwa na mabingwa hao wa Amerika Kusini katika mchezo huo wa kwanza wa Kundi B wa mashindano hayo. 

"Nafikiri tulianza mchezo taratibu, tukiwa na hofu kwa sababu tulijua tulikuwa tunacheza na timu bora," alisema Broos.

"Baada ya dakika 20, tulikuwa na uwezo wa kufungwa mabao matatu. Lakini baada ya hapo tulianza kurudi katika mchezo na kipindi cha pili tulicheza vizuri zaidi.

Kocha huyo Mbelgiji anaamini mabingwa hao wa Afrika wamepata cha kujifunza baada ya kipigo hicho kutoka kwa Chile.

"Bao la kwanza la Chile lilipatikana baada ya dakika 80 ni wazi zimetuhudhunisha kwa kuruhusu magoli hayo, lakini tunajivunia namna tulivyocheza kwa kiwango cha juu mchezo huu," alisema kocha huyo.