In Summary
  • Wanariadha wa Tanzania wanajiandaa na mashindano ya Madola yatakayofanyika Aprili

Kocha wa timu ya Taifa ya Riadha, Zakaria Barie amesema siku 45 za kambi kwa wanariadha wanaojiandaa na mashindano ya Jumuiya ya Madola itakayowekwa West Kilimanjaro wiki ijayo zinatosha.

Barie ni mmoja ya makocha wanne walioteuliwa na kamati ya Ufundi ya RT kuwa na kazi ya kukinoa kikosi hicho alisema pamoja na kuwa kambini siku 45, lakini kila mwanariadha alikuwa katika mazoezi siku zote.

 “Kitakacho kwenda kufanyika kwa hivi sasa ni kitu kidogo ambacho siyo kigeni kwao na siwezi kusema ni kitu gani tutaanza nacho kambini ila tutakapokutana na wenzangu ndio tutajua tunafanya nini kwa muda uliobaki”alisema Barie.

Aliongeza kuwa makocha wa klabu wanazotokea wanariadha hao ni msaada mkubwa kwani wamekuwa wakibeba mzigo huo kwa muda mrefu tangu wanariadha walipofuzu kwenda Madola.

Kuhusu matumizi ya chakula alisema wanariadha wanatumia vyakula vya kawaida kama binadamu wengine ndio maana hata wapishi wanaotumika ni wale wenye uzoefu na mambo ya lishe ili kuwasaidia wafukuza upepo hao.

Kocha Barie alikuwa kwenye Jopo la makocha la kuwanoa wanariadha walikwenda kwenye mashandano ya Olimpiki huko Brazil mwaka juzi, Mashindano ya Nyika yaliyofanyika Uganda mwaka jana pamoja na yale mashindano ya Dunia yaliyofanyika Agosti mwaka uliopita huko London.