In Summary
  • Kocha huyo aamenza vema kibarua chake Kenya kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu

Nairobi. Kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerr jana Jumatatu alijichora Tattoo yenye nembo ya klabu yake ya sasa  Gor Mahia ya Kenya katika mguu wa kushoto ikiwa ni ishara ya mapenzi yake baada ya kuiongoza kutwaa ubingwa wa Kenya.

Kocha huyo alichora nembo hiyo katika duka moja la kucholea tatoo jijini Nairobi na zoezi hilo lilichukua takribani dakika 40 tu kumalizika.

Mtaalamu wa kuchora Tattoo, Mark Moseti alisema alimchora nembo ya wastani, ambayo ilimgharimu kocha huyo kiasi cha 110,000 ya Tanzania.

Kocha Kerr alisema sababu kuu ya kuchora Tattoo ni kuweka kumbukumbu ya kuongoza Gor Mahia a.k.a Kogalo kutwaa ubingwa wa msimu wa 2017.

“Niliahidi jambo hilo miezi miwili iliyopita kwamba ningejichora iwapo tungeshinda taji. Nina Tattoo tatu kwenye mwili wangu, mbili za soka na moja ya mama yangu Gloria, ambaye atafika nchini (Kenya) wiki hii,” Kerr aliliambia Mwanaspoti.